- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kuhusu ununuzi wa Kahawa Mkoani Kagera lengo kuu la Serikali ni kuona wakulima wanapata bei nzuri wananufaika na zao lao la kiuchumi la kahawa tena wanalipwa kwa wakati ili kukidhi mahitaji yao mbalimbali ya kuwasomesha watoto na kujikimu kifamilia.
Ndiyo maana tangu msimu uliopita wa mwaka jana 2018 Serikali iliamua kuanzisha mfumo mpya wa kuhakikisha Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani Kagera havinunui kahawa bali vinakusanya kahawa ya Wakulima na baadae kuiuza kahawa hiyo kwaniaba ya wakulima na siyo vyama hivyo vikuu kufanya biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti wakati akizindua rasmi msimu wa ukusanyaji wa kahawa kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya KCU 1990 LTD na KDCU LTD mwaka huu Juni 29, 2019 Nkwenda Wilayani Kyerwa alieleza wazi kuwa mwaka huu 2019 atahakikisha wakulima wanapata malipo yao ya awali ya shilingi 1100/= kwa kila kilo ndani ya siku kumi baada ya mkulima kupeleka kahawa zake katika chama cha Msingi.
Pili, aliwaomba wakulima kuhakikisha wanafungua akaunti benki ili walipwe fedha zao kupitia Benki ili kupunguza mianya ya fedha ya mkulima kutumika isivyopangwa hasa kwa viongozi wa Vyama vya Msingi ambapo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini Bw. Japhet Justine aliweka wazi kuwa faida ya mkulima kulipiwa benki itamsaidia kuaminika kukopesheka kwasababu taarifa zake za kibenki zitaonesha mapato yake anayoyapata kwa msimu.
Tatu, Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwataka wanunuzi binafsi kuweka wazi bei zao za kahawa ili kama wapo tayari na kutoa bei inayomnufaisha mkulima wawasiliane na ofisi yake wapatiwe kahawa na siyo kwenda kwa wakulima mashambani kununua kahawa huko, hapo Serikali sasa inataka Mkulima asidhurumiwe wala kulipwa fedha kiduchu.
Julai 11, 2019 Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli akitokea Wilayani Karagwe pia alipigilia msumari kuwa Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa kuvipa Vyama Vikuu vya Ushirika Fedha ili vikusanye kahawa ya wakulima na kuiuza kwa kulenga kumunufaisha mkulima. Pia alitoa wito kwa wanunuzi binafsi kama wanataka kununua kahawa watoe bei nzuri na wamuone Mkuu wa Mkoa watanunua kahawa.
Kiukweli maoni mengi yamekuwa yakitolewa kutoka Wilaya zinazolima kahawa kwa wingi za Karagwe na Kyerwa kuwa wanunuzi binafsi waruhusiwe kutoka nchi jirani lakini ukiwauliza walalamikaji hao kwanini wanunuzi hao wanunue kahawa usiku tena kutoka kwa mkulima moja kwa moja na kupitisha kahawa hizo njia za panya na si kununua mchana na kupita mipaka halali hawatoi majibu.
Nakumbuka Mkuu wa Mkoa Gaguti akiwa anakagua mipaka Wilayani Kyerwa Juni 13, 2019 Mzee Johakhim John alilalamika kuwa wanunuzi binafsi waruhusiwe kutoka nchi jirani na Mhe. Gaguti alimweleza kuwa kama anaye mnunuzi ambaye yupo tayari kununua kahawa mchana amlete na aseme anataka tani ngapi na aseme bei yake lakini Mzee John alibaki kimya na alipoelezwa faida za mfumo mpya alibaki kuipongeza Serikali na kuomba iongeze Vyama vya Msingi vya kukusanyia Kahawa kutokana na umbali wa kuvifikia vilivyopo.
Katika suala hili la kahawa Serikali haijapiga marufuku wanunuzi binafsi bali utaratibu ufuatwe kodi ya Seriakli ilipwe tena stahiki mkulima alipwe vizuri kwa wakati na kwa kahawa yake ipimwe kwa kipimo sahihi ambacho ni mzani na si (visado) ambavyo ukijaza unaambiwa kilo moja kumbe kilo mbili nanusu hadi tatu, au (Rumbesa) unaambiwa kilo sitini kumbe kilo mia na zaidi.
Wakulima tufunguke macho Serikali nia yake ni nzuri kwani kuna mnunuzi atakwambia mwaka huu bei ya kahawa ni kiasi fulani jambo ambalo si kweli bali bei hotulewa na soko la dunia na ndiyo maana unapolipwa mwanzoni unaambiwa hayo ni malipo ya mwanzo ili kahawa ikishauzwa katika soko la dunia nyongeza ikipatikana mkulima anaongezewa.
Katika picha zifuatazo hapo chini unaweza kuona Wakuu wa Mkoa huu wa Kagera kwa vipindi tofauti wanavyoangaika na vipimo vya kupimia kahawa za Wakulima kama vipo sawa. Aliyewahi kuwa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu unamuona akihakiki mzani kwa kuhakiki uzito wake mwenyewe. Pili Mkuu wa Mkoa wa Kagera wa sasa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti unamuona akihakiki mzani hadi nukta (Point) za mkulima zisomwe katika mzani ili mkulima asiibiwe au kupunjwa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa