- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
PS3 Yazinoa Halmashauri Mkoani Kagera Juu ya Motisha Kwa Watumishi Ili Kuboresha Utoaji Huduma Kwa Wananchi
Mradi wa kuimarisha Mifumo katika Sekta ya Umma Tanzania (PS3) wawanoa watendaji na Waajiri Mkoani Kagera namna bora ya kuwamotisha watumishi wao katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili watumishi hao waweze kufikia malengo na matarajio ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo ya siku sita Mkoani Kagera yamewahusisha Wenyeviti, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wa Halmashauri za Wilaya mbili za Biharamulo na Kyerwa ambazo zipo katika awamu ya kwanza ya Mradi wa PS3 pamoja na Wakuu wa Idara katika idara za Utawala na Raslimali Watu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Kagera Kagera.
Mafunzo hayo yamelenga kuboresha utendaji na utoaji wa huduma bora kutoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda kwa wananchi ambapo mtumishi akipewa motisha mbalimbali anazozistahili hutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na mwananchi hupata huduma anayostahili kupata na kwa wakati.
Mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha Waajiri na Wakuu wa Idara hasa Idara za Utawala na Raslimali Watu kutoa motisha kwa watumishi wao jambo ambalo litawafanya watumishi hao kufanya kazi katika eneo lolote hata kama kuna changamoto za baadhi ya huduma za jamii mfano vijijini ambako huduma za maji na umeme hazijawafikia wananchi.
Akitoa ufafanuzi juu ya ufanisi wa mafunzo hayo Bw. Aloyce Msigwa kutoka PS3 Makao Makuu Dodoma alisema Mradi unalenga kuwakumbusha waajiri na wakuu wa idara juu ya utoaji wa motisha ili huduma kwa wananchi ziweze kuboreka lakini pia na kupunguza msongo wa mawazo kwa watumishi wakati wakitekeleza majukumu yao.
Akifunga mafunzo hayo Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Nesphory Bwana aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa Serikali ilishatoa mwongozo wa namna ya kuwahamasisha watumishi ili waweze kutoa huduma bora kupitia utoaji wa motisha.
“Mwongozo huo ulitolewa kupitia Sera ya Malipo na Motisha ya mwaka 2010 na upo muda mrefu lakini kwa sababu mbalimbali waajiri na hasa Mamlaka za Serikali za Mitaa wamekuwa wazito katika kubuni mbinu za kuutekeleza. Wakati mwingine jambo hili halitekelezwi siyo kwa sababu ya uwezo mdogo wa Halmashauri bali kwa sababu ya Uongozi husika kutokuona umuhimu wake na hivyo kutolipa kipaumbele.” Alisistiza Bw. Nesphory
Aidha, Bw. Nesphory alitoa wito kwa viongozi wote, watendaji na wanasiasa kubadilika na kulipa umuhimu jambo hilo kwa kuanza kulitengea bajeti kila mwaka kwa yale ambayo Halmashauri ina uwezo nayo.
Katika hatua nyingine Halmashauri za Wilaya za Biharamulo na Kyerwa ziliweza kupata fursa ya kuandaa mipango ya motisha kwa watumishi wao na pia mikakati ya kuitekeleza mipango hiyo. Ambapo pia Halmashauri hizo mbili ziliweza kubadilishana mipango hiyo ya motisha kwaajili ya ufanisi zaidi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa Oktoba 30, 2017 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna Diwani Athumani na yamefungwa leo Novemba 4, 2017.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa