- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Alphaxard Lugola awasili Mkoani Kagera na kuanza ziara yake ya siku saba kwa kutembelea Idara zilizoko chini ya Wizara yake ili kujionea utendaji kazi katika idara hizo ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano wa hadhara kusikiliza na kutatua kero za wananchi hasa zinazohusu Idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri Kangi Lugola mara baada ya kuwasili Mkoani Kagera Januari 2, 2019 aliitembelea Idara ya Huduma za Uangalizi inayosimamia utekelezaji wa adhabu mbadala nje ya Magereza. Adhabu mbadala kwa kifupi ni aina ya hukumu itolewayo na Mahakama kwa mtu aliyepatikana na hatia kwa kosa la jinai ambapo kisheria mfungwa hupewa adhabu ya kufanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii bila ya malipo kwa faida ya jamii.
Akiwa Katika ofisi ya Idara ya Huduma za Uangalizi yenye mtumishi mmoja Mkoani Kagera Waziri Kangi Lugola baada ya kusomewa taarifa ya idara hiyo alisema kuwa idara hyo ipo chini ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani ya nchi na katika Idara zenye watumishi wengi ni pamoja na Idara hiyo yenye Watumishi 160 lakini shughuli zake hazifahamiki na tija yake ni ndogo sana kwa wananchi.
“Idara hii zamani ilifahamika kama Bwana Huruma kwani ilikuwa inawasaidia wafungwa waliokuwa wanaonesha mwenendo mzuri katika Magereza kufungwa kifungo cha nje lakini baada ya kubadilishwa jina wananchi wengi haifahamu,” Alifafanua Waziri Kangi Lugola. Aidha, Waziri Lugola alitembelea Idara za Polisi, Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Idara ya Vitambulisho vya Taifa NIDA na kujionea utendaji kazi wa idara hizo Mkoani Kagera.
Mkutano wa Hadhara
Akiwa katika Mkutano wa hadhara uwanja wa Uhuru Manispaa ya Bukoba Waziri Kangi Lugola aliongea na wananchi na kusikiliza kero mbalimbali hasa kero kubwa ililihusu Jeshi la Polisi Mkoani Kagera katika utendaji wake wa kazi hasa katika Upande wa usalama barabarani na Bodaboda. Waendesha Pikipiki maarufu kama Bodaboda walililalamikia Jeshi la Poilisi kuwakamata bila kuvaa sare za Jeshi hilo, kuwakimbiza na kuwasababishia ajali zinazopelekea ajali mbaya na pengine kupelekea vifo.
Akitoa ufafanuzi Waziri Kangi Lugola alisema kuwa Jeshi la Polisi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi wakiwa wameva sare za Jeshi hilo na hairuhusiwi kwa Askari Polisi yeyote kumkata Bodaboda bila kuvaa sare za Jeshi la Polisi kwani wamesababisha hata majambazi kuwadhuru Bodaboda wakijifanya ni Askari wa Jeshi la Polisi na kuwanyanganya Pikipiki zao.
Waziri Kangi Lugola alisema kuwa Jeshi la Polisi wanatakiwa kulinda raia na mali zao na si vinginevyo ambapo alitoa mfano kwenye ardhi kuwa wananchi wanyonge wamekuwa wakidhurumika sana katika upande wa ardhi lakini Jeshi la Polisi wapo na hawatekelezi wajibu wao bali matajiri wenye fedha wanaendelea kuwanyanyasa wananchi masikini kwa kuchukua ardhi zao na kuzitumia katika ujenzi.
Pia Waziri Kangi Lugola aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa wazalendo kwa kutowapa hifadhi wahamiaji haramu na kutoa msaada kwa Serikali kuisaidia Idara ya Uhamiaji kwa kutoa taarifa pale wanapogundua kuwa kuna wahamiaji haramu katika maeneo yao kwani Mkoa wa Kagera ni mkoa ambao unapakana nachi nyingi.
Katika hatua nyingine Waziri Kangi Lugola alitoa ufafanuzi mambo makuu mawili ambayo aliwahi kuyasema hapo awali. Kwanza, Askari wa Usalama Barabarani kukamata gari na kumhesabia dereva makosa zaidi ya moja na kila kosa kutozwa faini ya shilingi 30,000/=, Waziri Kangi Lugola alisema kuwa gari likibainika kuwa lina makosa zaidi ya moja dereva anatakiwa kulipia kosa moja tu la ubovu wa gari lakini si kila kosa kulipia faini tajwa hapo juu.
Pili, Waziri Kangi Lugola alitoa ufafanuzi juu ya suala la mabasi ya abiria kuanza safari alfajiri saa 11:00 badala ya saa12:00 asubuhi. Waziri Kangi Lugola alisema suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na Serikali na baada ya Januari 10, 2018 Serikali itatoa msimao wa suala hilo na utaratibu mzuri wa utekelezaji.
Waziri Kangi Lugola yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya siku saba kuanzia tarehe 2.01.2019 hadi 8.01.2019 ambapo atafanya ziara katika Wilaya zote za Mkoa kwa kufanya Mikutano ya Hadhara kuongea na wananchi na kutatuta kero zao pia kuongea na watumishi wa Idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa