- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika siku yake ya kwanza ziarani Mkoani Kagera aeleza na kufafanua juu ya mfumo mpya wa ununuzi wa kahawa na jinsi Serikali ilivyojipanga kuhakikisha mkulima ananufaika pia mfumo mpya utakavyobershwa katika Msimu wa Kahawa wa mwaka 2019 ili Vyama Vikuu vya Ushirika visifanye biashara ya Kahawa bali Wafanyabiashara tu..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza hayo Oktoba 6, 2018 kwenye kikao cha wadau wa Kahawa Manispaa ya Bukoba katika ukumbi wa Hoteli ya ELCT Bukoba mara baada ya kupata taarifa fupi kutoka kwa Waziri wa Kilimo Dk.Charles Tizeba kuhusu ukusanyaji, uuzaji wa Kahawa na malipo ya wakulima pamoja na changamoto za mfumo mpya katika uuzaji wa Kahawa Mkoani Kagera.
Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba alimweleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao hicho kuwa changamoto kubwa iliyojitokea katika Msimu huu wa 2018 kwenye zao la Kahawa Mkoani Kagera Moja ni Kahawa kushuka bei katika soko la dunia kuliko ilivyowahi kushuka kwa miaka 12 iliyopita kutokana na wazalishaji wakubwa wa Kahawa duniani kuzalisha Kahawa kwa wingi sana.
Pili ni Kahawa kununuliwa kwa kiwango kidogo na kusababisha mlundikano wa kahawa iliyokusanywa kutoka kwa wakulima katika maghara ya Vyama Vikuu vya Ushirika na kusababisha Wakulima kutolipwa fedha zao kwa wakati ambapo jumla ya tani 11,000 za Kahawa bado zipo magharani. Tatu Waziri Tizeba alisema kuwa ni propaganda za kuishusha Kahawa bei iliyokuwa ikiendelea kwa baadhi ya wafanyabiashara ili kunufaika kwa kununua Kahawa kwa bei ndogo.
Baada ya kupata taarifa hiyo Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa Serikali inasisitiza uchumi wa viwanda ili Tanzania iweze kusonga katika uchumi wa kati ambapo mazao ya sita ambayo Serikali imeyawekea mkakati wa kuhakikisha yanapewa kipaumbele na kuchakatwa katika viwanda ili kuleta mapinduzi katika kilimo na kwenye sekta ya Viwanda kwa kujenga viwanda vya kusindika au kuongeza thamani ya mazao hayo.
Akitaja mazao hayo Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa Pamba, Chai, Tumbaku, Korosho, Kahawa na Mchikichi ndiyo mazao ya kimkakati kwa sasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda. Aidha, alisema katika maeneo yote mfumo wa kununua na kuuza mazao hayo unaenda vizuri isipokuwa zao la Kahawa Mkoani Kagera bado lina shida kubwa kutokana na kutokubalika kwa mfumo huo mpya ulioletwa na Serikali kukusanya na kuuza Kahawa kutokana na baadhi ya watu kujikita mizizi kwenye “Obutura”.
Mfumo Mpya wa Kuuza Kahawa
“Nimezunguka kote nchini na mfumo wa kuuza mazao yote ya kimkakati umekubalika maeneo yote kwenye Pamba, Korosho, Ufuta lakini Kagera imeshindikana kwasababu ya watu wachache kufanya biashara ya “Obutula”. Niwashauri wakulima wa Kagera kubadilika katika mfumo wenu wa kutaka malipo ya awali na ndiyo inayosababisha matatizo haya yote, lakini tukiacha mazoea ya kulipwa kwanza tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa na lazima tusubiri malipo ya pamoja. “Alieleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa ili kutatua changamoto ya malipo ya wakulima kuchelewa na kahawa kuendelea kukaa kwenye maghara tani 11,000 alimua kukaa na Wafanayabiasha wa Kahawa ili kuwasikiliza na kukubaliana nao namna bora ya kununua Kahawa ambapo alikubaliana nao katika kikao chake cha awali kuwa watanunua kahawa yote tani 11,000 ambayo Vyama Vikuu vya Ushirika tayari vimeikusanya kwa wakulima na ipo katika mghara ya Vyama hivyo.
Serikali Kuboresha Mfumo Wa Ununzi Msimu wa 2019
Waziri Mkuu alisema kuwa kuanzia msimu ujao wa Kahawa wa Mwaka 2019 minada yote ya uuzaji wa Kahawa haitafanyika Moshi Mkoani Kilimanjaro bali itafanyika Mkoani Kagera. Pili alisema lazima tozo za Kahawa zifanane katika Vyama vya Ushirika na alitolea mfano wa KDCU LTD na KCU 1990 LTD kuwa tozo zao zinatofautiana wakati zao la Kahawa ni moja na linatoka mkoa mmoja.
Chama Kikuu cha KCU 1990 LTD kati ya tozo 23 zilizokuwepo awali kimepunguza tozo tano tu na kubaki na 18 wakati KDCU LTD wao wamepunguza tozo tatu tu na kubaki na tozo 20. Kwanini zitofautiane wakati Kahawa ni ileile na inatoka Mkoa wa Kagera. “Aliuliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa”
Vyama Vikuu Kutofanya Biashara Ya Kahawa Msimu wa 2019
Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa alisema kuanzia Msimu wa 2019 Vyama vyote Vikuu vya Ushirika havitarusiwa tena kufanya biashara ya Kahawa ambapo vimekuwa vikisababisha hasara kubwa kwa ubadhirifu wa fedha na kusabisha Serikali kulipa madeni ya Vyama hivyo na watakaoruhusiwa kufanya biashara ya Kahawa ni Wafanyabiashara tu.
Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo haitatoa tena fedha kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika bali kwa Wafanyabiashara tu wa kununua na kuuza Kahawa. Viongozi wa Vyama vya Ushirika watasimamia utaratibu wa wafanyabiashara kununua na kuuza Kahawa Katika Vyama vya Msingi na kuvisimamia Vyama hivyo katika mfumo huo mpya vilevile kutoa vibali vya kusafirisha Kahawa nje ya nchi kwa wafanyabiashara.
Katika Mfumo huo mpya wa kuuza Kahawa ya Wakulima Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa wakulima na wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanafungua akaunti katika Benki za NMB na CRDB ili malipo yao yawe yanapitia katika benki hizo badala ya kulipwa fedha mkononi na alisisitiza kuwa Wanankagera kuwa ni waelewa hawahitaji kusukumwa katika hilo.
Jukumu la vyama vya Msingi ni kuhakikisha vinawatambua wakulima wake kila mahali walipo na kujua mkulima mmoja mmoja ana uwezo gani wa kuzalisha Kahawa ili mfumo wa ununuzi ukiwa mzuri mkulima aweze kunufaika na kuboresha shamba lake na kuvuna zaidi.
Akifafanua juu ya Vyama Vikuu vya Ushirika kufanya Biashara Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Chama Kikuu chaUshirika KCU 1990 LTD kinadaiwa mabilioni ya fedha na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizokuwa za Serikali kutokana chama hicho kujiingiza kwenye biashara. Pili alisema kuwa chama hicho kutokana na kukopa fedha sehemu mbalimbali bila kulipa kina kesi zaidi ya 10 Mahakamani nyingi zikiwa za Madai.
Magendo Ya Kahawa Obutura
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia magendo ya kahawa katika maeneo yao kikamilifu. Aidha, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa Agustine Olomi kuwaonya Askari walio chini yake hasa Katika Wilaya ya Kyerwa kuacha tabia ya kusindikiza kahawa za Magendo bali wafanya kazi yao kama sheria inavyowaelekeza.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa onyo kwa Viongozi wa Serikali na Watumishi kutojihusisha kwenye biashara ya magendo hasa katika Wilaya ya Kyerwa na kama hawataacha tabia hiyo Serikali itawachukulia hatua za kisheria mara moja.
Katika Hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim majaliwa alivitembelea Viwanda vya BUKOP na Kiwanda cha TANICA vilivyopo katika Manispaa ya Bukoba na kuongea na watumishi wa viwanda hivyo na kupongeza Menejimenti za Viwanda hivyo kuajili watanzania zaidi ya 1800.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa