- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa aendelea na ziara yake Mkoani Kagera Wilayani Kyerwa na Karagwe ambapo Kyerwa alitembelea Chama cha Msingi Nkwenda na Kumuagiza Mkuu wa Mkoa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanachukua hatua mara moja kukomesha magendo ya Kahawa Wilayani Kyerwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa onyo kali kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kyerwa kuhakikisha anakomesha magendo ya Kahawa na kuacha tabia ya kushiriki kusindikiza kahawa za magendo kutoroshwa kuelekea nchi jirani wakati jukumu la Jeshi la Polisi ni kudhibiti magendoi ya kahawa.
“OCD (Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kyerwa) wewe na baadhi ya Maafisa wenzako mnalichafua Jeshi la Polisi kwa kusindikiza kahawa za magendo, acha tabia hiyo mara moja tutakuvua vyeo na kusimamisha kazi wakati bado familia yako inakutegemea. OCD simamia kahawa, OCD simamia Kahawa, OCD simamia Kahawa.” Alimuonya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kyerwa Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa.
Aidha, katika hatua nyingine alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustine Olomi kuhakikisha wanashughulika na Wilaya ya Kyerwa kwa kukomesha Magendo ya Kahawa katika Wilaya ya Kyerwa ili kahawa iuuzwe kwa mfumo halali wa Ushirika na kumnufaisha mkulima moja kwa moja.
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alirudia kauli ya Serikali alaiyoitoa Oktoba 6, 2018 akiwa Manispaa ya Bukoba ya kuuboresha mfumo mpya wa kunuanua kahawa Mkoani Kagera na kusema kuwa kuanzia msimu ujao wa mwaka 2019/2020 Mnada wa Kahawa utafanyika Mkoani Kagera ili kupunguza gharama za makato kwenye fedha za Wakulima.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahakikishia wananchi ambao tayari wamekusanya kahawa yao kwenye Chama Kikuu cha Ushirika KDCU Limited na hawajalipwa fedha zao kuwa watalipwa kwani Benki ya Maendeleo ya Kilimo tayari imetoa fedha kwa chama hicho ili kuwalipa wakulima hao. Pia alikiagiza Chama cha Msingi Nkwenda ambacho alitembelea kiwanda chake cha Kukoboa kahawa kuwa kitangaze mara moja mnada wa kahawa ambayo tayari wameikusanya ili kuwalipa Wakulima.
Vile vile Mbunge wa Kyerwa Innocent Bilakwate na Mbunge wa Viti Maalum Oliver Semguruka waliwasilisha kero za wananchi katika Sekta za Maji, Afya, Elimu na Ardhi ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini mfano kwa kuongeza ujenzi wa vituo vya afya, madawa na watumishi.
Aidha, katika Sekta za Maji na Ardhi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahidi wananchi wa Wilaya ya Kyerwa kuwa atawatuma Mawaziri wa Sekta hizo kwenda Wilayani Kerwa kusikiliza kero hizo kuzitatua na kuchukau hatua kama kutakuwa na uzembe uliofanyika kwa kusababishwa na Watendaji wa Serikali.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alitembelea kiwanda cha KADERES cha kukoboa kahawa chenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5 kinachomilikiwa na Mwekezaji Leonard Kachebonaho Wilayani Karagwe na kupongeza juhudi za mwekezaji huyo za kuajili wananchi wenzake na kupunguza uhuhitaji wa ajira kwa vijana nchini.
Kiwanda hicho cha KADERES kinakoboa kahawa na kuzipanga kwa madaraja, pia kinaajili wananchi wazawa 30 hadi 200 na kinawahudumia wakulima 1800 ambapo kwa msimu huu wa mwaka 2018/2019 kitaanza kulipa wakulima waliokusanya kahawa yao kwa kiasi cha shilingi 1,700/= kwa kilo na baadae wakulima hao watalipwa shilingi 100/= na kukamilisha jumala ya shilingi 1,800/=.
Mara baada ya kukitembelea kiwanda hicho Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuunga Mkono wawekezaji katika Sekta ya Viwanda kwa kusema kuwa viwanda vina mambo makuu muhimu matatu. Kwanza kuboresha mazao mbalimbali ya kilimo na biashara kwa kuyaongezea thamani, Pili viwanda vinpunguza sana tatizo la ajira kwa kuajili wananchi wengi kwa wakati mmoja.
Tatu, ni kutoa fursa kwa wananchi wazawa Watanzania kujifunza teknolojia na ujuzi wa kuendesha viwanda wazawa wenyewe bila kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimalizia kuwa Viwanda vimeondoa vijiwe vya vijana kwa kutoa ajira nyingi kwa vijana nchini. Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa alimalizia ziara yake Wilayani Karagwe kwa kuongea na wananchi katika Mkutano wa hadhara Uwanja wa Changarawe Kayanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa