- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti anawataarifu Wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafanya ziara ya Siku nne hapa Mkoani kwetu Kagera kuanzia tarehe 6 Oktoba, 2018 hadi tarehe 9 Oktoba, 2018.
Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kuwasili Mkoani kwetu tarehe 06/10/2018 siku ya Jumamosi saa 7:00 Mchana katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Mhe. Waziri Mkuu mara baada ya kuwasili Mkoani atapokea taarifa ya Mkoa na mara baada ya kupokea taarifa hiyo ataanza ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na atatembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo Maruku, atatembelea pia Kiwanda cha kukoboa kahawa cha BUKOP LTD na Kiwanda cha TANICA katika Manispaa ya Bukoba na ataongea na wadau mbalimbali wa Kahawa pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Kagera katika Ukumbi wa Hoteli ya ELCT Bukoba. Tarehe 07/10/2018 Mhe. Waziri Mkuu ataendelea na ziara yake Wilayani Kyerwa kwa kutembelea AMCOS ya Nkwenda baada ya hapo ataelekea Wilayani Karagwe ambapo atatembelea Kituo cha Afya Kayanga, Kuzindua Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha KADERES na kuongea na wananchi katika Mkutano wa Hadhara Uwanja wa Changarawe Kayanga.
Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera tarehe 08/10/2018 Wilayani Muleba na Biharamulo ambako atetembelea Shamba bora la Kahawa, Kituo cha Afya Kimeya na kuongea na Watumishi na Wananchi. Aidha, Mhe. Waziri Mkuu ataelekea Biharamulo ambako atatembelea Mgodi wa STAMIGOLD na kuongea Wananchi katika Mkutano wa Hadhara Nyakanazi.
Mhe. Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake Mkoani Kagera tarehe 9 Oktoba, 2018 atakapopokea Vyumba vya Madarasa Katika Shule ya Msingi Nyakato na Kashozi vilivyojengwa kwa msaada wa Ubalozi wa nchi ya Japan baada ya kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi mwaka 2016. Pia atetembelea kiwanda cha Kahawa cha Amir Amza na kuongea na Wananchi wa Manispaa ya Bukoba na Viunga vyake Katika Uwanja wa Uhuru (Mayunga).
Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti anawaomba wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kuonesha ushirikiano, bashasha na ukarimu kwa Mhe. Waziri Mkuu kwa kufika kwa wingi katika maeneo yaliyotajwa kumpokea na kumkaribisha katika Mkoa wetu wa Kagera. Pia Wilayani ambako Mhe. Waziri Mkuu atatembelea wananchi wanahamasishwa kufika kwa wingi kumsikiliza kwa muda utakaokuwa umepangwa kuongea na wananchi katika Mikutano ya Hadhara.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti anatoa wito kwa wananchi kudumisha umoja, amani na mshikamano wakati wote wa ziara ya Mhe. Waziri Mkuu na kutojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa kuwa Vyombo vya Ulinzi na Usalaama vipo tayari muda wote kushughulika na wananchi wasiopenda amani. Aidha, kama ilivyo kawaida ya wananchi wa Mkoa wa Kagera kudumisha usafi wa mazingira tunaomba kudumisha utamaduni huo ili kuweka maeneo yetu katika hali ya usafi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa