- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Kilimo Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage wafanya ziara ya siku tatu Mkoani Kagera kuwaelimisha Wakulima, Viongozi Vyama vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika kuhusu ukusanyaji wa kahawa ya wakulima, bei ya kahawa, malipo ya awali na malipo ya pili kwa Mkulima.
Wakiwa Mkoani Kagera Mawaziri hao Tizeba na Mwijage kuanzia Julai 10 hadi 12, 2018 walifanya ziara za pamoja katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Muleba kuwaelimisha wakulima na viongozi mbalimbali hasa kuhusu umuhimu wa Ushirika na bei ya kahawa iliyokuwa inawachanganya wananchi na kupelekea kuuza kahawa zao kwa njia za magendo.
Ushirika Kuknunua Kahawa ya Wakulima.
Waziri Tizeba akiwa Mkoani Kagera alitoa ufafanuzi kuhusu Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani hapa vya KCU 1990 LTD na KDCU LTD kuwa wananchi hawatakiwi kuvitafsiri kuwa vinanunua kahawa bali vyama hivyo vikuu vinakusanya kahawa ya wakulima na kuipeleka kahawa hiyo katika Mnada wa Soko la dunia kupata bei.
Bei ya Kahawa, Malipo ya Awali na Malipo ya Pili
Waziri Tizeba na Mwijage walitoa ufafanuzi wa bei kuwa bei ya kahawa inajulikana mara baada ya kahawa kuuzwa kwa mnada katika Mnada wa Soko la Dunia. Pia ilifafanuliwa kuwa kwasababu Mkoa wa Kagera ulizoea mfumo wa kupata malipo ya awali Serikali iliamua kuwa kabla ya kahawa kuuzwa katika Mnada wa Soko la dunia mkulima alipeleka kahawa yake katika chama cha msingi alipwe malipo ya awali kila kilo moja shilingi 1000/=
Mara baada ya kahawa kuuzwa kwenye Mnada wa Soko la dunia na bei halisi kujulikana na makato ya gharama mbalimbali kukatwa mkulima atapata malipo ya pili ili kukamilisha bei halisi ya kahawa kwa mkulima. Mnada wa Soko la Dunia ulifanyika Julai 12, 2018 na bei ilifikia Dola (1.8 USD) ambayo ilipobadilishwa katika shilingi kwa siku hiyo bei ilikuwa ni shilingi 4,032/= hiyo ndiyo bei ya kahawa kabla ya makato.
Makato na Kodi Mbalimbali
Waziri Tizeba alitoa ufafanuzi kuwa Serikali imepunguza makato ya kodi mbalimbali katika zao la kahawa na mwaka huu 2018 makato ya kodi yamepunguzwa kutoka shilingi 1,700/= hadi shilingi 490/= tu ili mkulima aweze kunufaika kwa kupata bei kubwa katika zao la kahawa na kuinua uchumi wao na uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Usajili wa Wakulima na Ulipaji wa Fedha za Awali kwa Wakulima
Kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika ulipaji wa fedha za awali kwa wakulima Waziri Tizeba aliagiza kuwa hakuna sababu ya Vyama vya Ushirika kuchelewesha malipo ya wakulima kwani vyama hivyo tayari vimepewa fedha na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Mkulima anatakiwa kulipwa malipo ya awali mara tu anapowasilisha kahawa yake kwenye Chama cha Msingi.
Aidha, Waziri Tizeba aliagiza Makarani wa Vyama vya Msingi kuhakikisha wanatumia busara kuwalipa fedha taslimu wakulima watakaowasilisha kahawa kidogo, wazee na wakulima walio katika maeneo yasiyokuwa na mitandao ya simu ili kuwaondolea usumbufu wa kupata fedha zao. Lakini kwa wakulima wenye kiasi kikubwa cha kahawa walipwe kwa njia ya benki kwa kuzingatia sheria ya fedha nchini.
Utata wa Bei ya Kahawa Kuwa Nzuri Nchi Jirani
Katika kuondoa utata na mkanganyiko wa bei ya Kahawa Mkoani Kagera na nchi jiarani ya Uganda Waziri wa Kilimo Chales Tizeba na Waziri Mwijge walikutana na Waziri wa Ushirika wa Uganda Mhe. Frederick Ngobi Mtukula Wilayani Missenyi ili kujua bei ya kahawa katika nchi ya Uganda na kama ikionekana bei ni nzuri kuliko Tanzania wakulima watafutiwe soko katika nchi hiyo.
Katika Kikao hicho Waziri wa Ushirika Nchini Uganda Frederick Ngobi alisema kuwa kahawa nchini Uganda inauzwa shilingi 2000 fedha za Kiganda lakini pia alisema kuwa tatizo la Obutura limekita mizizi sana nchini kwake na wakulima hawanufaiki kabisa na zao la kahawa bali watu wachache sana wanaojihusisha na biashara ya Obutura.
Naona mfumo wa ushirika wa kwenu (Tanzania) ni mzuri sana wakulima wenu wananufaika kwa kahawa yao. Ninaomba kuja kwenu kujifunza Vyama vya Ushirika vinafanyaje katika kufanya kazi ili mkulima anufaike. Kahawa kwetu imekuwa shida wakulima wanauza kwa njia ya Obutura na unapofika msimu hawapati kitu. Alifafanua Waziri Ngobi.
Waziri Mwijage na Tizeba walimueleza kuwa kama kuna Mganda yeyote ambaye anaweza kununua kahawa kutoka Mkoani Kagera kwa kufuata taratibu zote za kisheria bila kupita kwa wakulima kununua obutura kwa njia za magendo na bei inayoizidi ya Tanzania anakaribishwa kuja kununua kahawa. Ikumbukwe kuwa kahawa inauzwa kwenye soko la Mnada wa Dunia duniani kote kwahiyo Waganda hawana soko lao peke yao.
Malipo ya Awamu ya Tatu
Waziri wa Kilimo aliwahakikishia wakulima Mkoani Kagera kuwa kutakuwepo na malipo ya awamu ya tatu kwani mara baada ya kahawa kukoborewa huwa kunabaki kahawa chafu ambayo huuzwa mwisho wa msimu. Waziri Tizeba alisema kuwa hiyo siyo mali ya Vyama vya Ushirika bali mali ya wakulima kwahiyo inapouzwa wakaulima wanatakiwa kupata fedha zao ambazo Serikali itazisimamia kuhakikisha zinalipwa kwa wakulima.
Agizo la Waziri Tizeba
Kutokana na KCU 1990 LTD kufanya maandalizi ya msimu kwa gharama ya shilingi milioni 75 na Chama cha Ushirka cha KDCU LTD kutumia bilioni 1.3 alitoa agizo kwa Viongoz wa KDCU LTD kuhakikisha wanarudisha fedha ambazo zimetumika kibadhilifu kabla tume haijapitia hesabu zao vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa viongozi hao mara baada ya ukaguzi wa hesabu hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu mara baada ya ziara hiyo alitoa msimamo wa Serikali ya Mkoa kuwa hakutakuwa na mwananchi yeyote ambaye ataruhusiwa kuuza kahawa yake bila kupitia ushirika. Mhe. Kijuu alisema kuwa anataka kuona mkulima wa Kagera anatajirika kutokana ka kilimo cha kahawa na si vinginevyo. Pia alisema kwa yeyote atakayejaribu kufanya mageno ataona cha mtema kuni.
Aidha, Mhe. Kijuu alisema kuwa Mkoa utaanza kufanya uchunguzi wa fedha ya kahawa chafu iliyokuwa ikiuzwa kwa miaka 22 baada ya msimu ilikuwa inapelekwa wapi na Vyama vya Ushirika ili kuchukua hatua kwa waliohusika kutafuna fedha hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa