- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mwigulu Azindua Uandikishaji Wa Vitambulisho vya Taifa Kagera,
Aagiza Jeshi la Polisi Kuchunguza Mauaji Nchini na Kutoa Taarifa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Lameck Nchemba azindua rasmi zoezi la uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa Mkoani Kagera katika Kijiji cha Kasindaga Kata Kabitembe Wilayani Muleba leo Februari 16, 2018.
Katika uzinduzi huo Waziri Mwigulu aliwasisitiza wananchi kuhakikisha kila mmoja kuanzia umri wa miaka 18 nakuendelea kujiandikisha au kutambuliwa na kusajiliwa kwaajili ya kupata kitambulisho cha Taifa ambacho ni muhimu sana kwa kila Mtanzania kwa maisha ya kila siku.
Waziri Mwigulu alisema kuwa Kitambulisho cha Taifa ni muhimu sana kwa masuala ya kiusalama ambapo kila mwananchi atatambuliwa, Wakimbizi wote watatambuliwa na wale wote wanaotoa huduma za kiubalozi watatambuliwa na hakuna Mtanzania ambaye anatakiwa kubaki bila kutambuliwa.
Pia Waziri Mwigulu amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa na wivu wa uzalendo na nchi yao na mkoa wao pia kwa kutoa taarifa sahihi kwa wasio raia wa Tanzania kwa kuwa Kagera kuna vivutio vingi na unapakana na nchi nyingi jambo ambalo linawavutia watu au wahamiaji haramu kuingia nchi jirani.
“ Katika Mahabusu za Mkoa wa Kagera kuna waharifu wenye kesi za uharifu wa kikatili kuliko mahabusu za mikoa mingine lakini ukichunguza kwa undani utagundua wahalifu hao siyo Watanzania bali ni kutoka nchi za jirani ambapo hawana huruka za Kitanzania bali ukatili tu,” Alitoa mfano Waziri Mwigulu.
Katika Hatua nyingine Waziri Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Simon Sirro kutumia vyombo vyake vyote vya uchunguzi kuhakikisha anachunguza mauaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini (Akitolea mfano wa Kijana aliyeuawa Kinondoni wa chama cha CHADEMA) na baada ya uchunguzi Jeshi hilo litoe taarifa kwa wananchi ili kujua chanzo cha mauaji hayo.
Kwaniaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Hamelore M. Manyanga ambaye ni Kamishna wa Huduma za Sheria katika uzinduzi huo alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa sahihi wakati zoezi la utambuzi na usajili wa Vitambulisho vya Taifa likiendelea. Pia aliwaasa watendaji kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa katika zoezi hilo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuli kwa atakayebainika.
Aidha, Bw. Alphonce Malibicha Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Vitambulisho vya Taifa kwaniaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alisema kuwa wananchi wanaotakiwa kusajiliwa ni umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na raia wa Tanzania . Pia alisema kuwa uandikishaji unaendelea katika Mikoa 19 sasa Tanzania Bara na Kagera sasa imeongezeka baada ya kufanyika uzinduzi rasmi.
Bw. Malibicha alizitaja faida za Vitambulisho vya Taifa kuwa ni pamoja na huduma mbalimbali za kijamii, Vitambulisho vya Taifa vitatumika katika kusajili Makampuni ambapo mmiliki taarifa zake lazima zionekane kwenye kitambulisho, Vitatumika wakati wa kupata Hati ya kusafiria, Vitatumika katika mifuko ya Hifadhi za jamii katika kutoa huduma za mafao kwa wananchama wake pia na kubaini Wahamiaji Haramu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu katika uzinduzi huo alitoa maagizo kwa Watendaji wa ngazi zote kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kufanikisha zoezi la uandikishaji kwa kusimamia zoezi zima hasa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya chini ya Wenyeviti wake Wakuu wa Wilaya.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Kijuu alitoa wito kwa watendaji kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika zoezi hilo kwani wakibainika hatua kali zitachukuliwa mara moja. Pia aliwaasa wananchi kuhakikisha wahudhuria kujiandikisha kwa muda watakaopewa na wasisubiri muda wa mwisho na kusababisha msongamano.
Mwisho Mh. Kijuu aliwaomba viongozi wa dini kuwahamasisha waamini wao kujiandikisha kila mmoja. Pia alisistiza kuwa zoezi la uandikishaji lisichukuliwe kidini wala kisiasa kwa kuwapotosha wananchi na mwisho wake baadhi yao wakabaki bila kujisajili na kupata Vitambulisho vya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa