- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Serikali Mkoani Kagera Yakamata Tani Samaki Wenye Thamani ya Zaidi ya Milioni 200 Waliovuliwa Kwanjia Haramu Kisiwani Lubili
Serikali Mkoani Kagera yakamata na kutaifisha tani 65.6 za samaki aina ya sangara wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 waliovuliwa kwa njia haramu na kukaushwa kwa chumvi (samaki hao wanajulikana kwa jina maarufu kama kayabo) ambao walikuwa wanaandaliwa tayari kusafirishwa kwenda nchi za nje kwa ajili ya kuuzwa.
Samaki hao waliovuliwa kwanjia haramu ni chini ya sentimeta 50 na juu ya Sentimeta 85 yaani samki watoto na samaki wazazi ambao hawaruhusiwi kishera kuvuliwa na walikamatwa katika Kisiwa cha Lubili Wilayani Muleba tarehe 30.12.2017 na kusombwa kuletwa katika kituo cha Maendeleo ya Uvuvi Kagera.
Kaimu Mkurugenzi idara ya Maendeleo ya Uvuvi Bi Mwanaidi Mlolo akiambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kujionea samaki hao katika kituo cha Maendeleo ya Uvuvi Kagera Januari 6, 2018 alisema samaki hao walivuliwa kinyume na sheria namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009. Ambapo pia sheria hiyo inatoa mamlaka ya kutaifisha vifaa vyote vilivyotumika katika zoezi zima la uvuvi haramu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akikagua tani 65.6 za samaki hao (Kayabo) katika kituo cha Maendeleo ya Uvuvi Kagera Januari 6, 2018 alisema kuwa samaki hao walivuliwa kwanjia haramu na walitarajiwa kutoroshwa kupelekwa nchi jirani kuuzwa bila kulipiwa mrahaba wa Serikali.
Waziri Mpina aliagiza samaki hao wauzwe kwa njia ya mnada kwa wafanyabiashara wenye vibali na leseni za kusafirisha samaki (kayabo) nje ya nchi ili Serikali iweze kupata mapato yake. Aidha, alitoa rai kwa wafanyabiashara wa samaki kufuata kanuni, taratibu na sheria katika kufanya biashara zao na bila kufanya uharibifu kwa kufanya uvuvi haramu.
Agizo, Mhe. Mpina aliwaagiza Watendaji chini ya Wizara yake kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara atakayekwenda kuhuwisha leseni yake ili kupata leseni mpya lazima mfanyabiashara huyo awe na kibali cha kulipia kodi (Tax Clearence) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Kwa kuwa leseni za uvuvi hutolewa kila mwaka mwezi Januari, wafanyabiashara ambao bado hawajaomba leseni upya lazima waje na kibali cha kulilipa kodi (Tax Clearance) ndipo wapate leseni mpya. Aidha, kwa ambao tayari walikuwa wamepata leseni mpya wahakikishe wanawasilisha vibali vyao vya kulipia kodi ndipo wataendelea kuruhusiwa kufanya biashara ya samaki,” alisistiza Waziri Mpina.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu alitoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kutoa taarifa walipojificha wahusika waliovua samaki hao katika Kisiwa cha Lubili ili Serikali iweze kuwachukulia hatua mara moja. Pia Mkuu wa Mkoa alisistiza kuwa pamoja na wahusika wa tukio hilo kutoroka lakini Serikali ina mkono mrefu itaweza kuwakamata na kuwafikisha katika mikona ya sheria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa