- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Kalemani Aiagiza Tanesco Kagera Kutumia Bilioni 6.5 Kuhakikisha Miundombinu Inarekebishwa Kupata Umeme wa Uhakika
Waziri wa Nishati Medard Kalemani asema Mkoa wa Kagera hauna shida ya uhaba wa umeme isipokuwa changamoto kubwa ni ubovu wa miundombinu ya umeme ambayo inakuwa imechoka au kupata hitilafu kama transifoma kuharibika au nguzo kuoza na kuanguka lakini umeme upo wa kutosha na ziada hasa Kagera.
Waziri Kalemani aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Kagera Juni 10, 2018 alipofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kusaini kitabu cha wageni ambapo alimwagiza Meneja waTANESCO Mkoa wa Kagera Francis Maze kuhakikisha anatumia shilingi bilioni 6.5 zilizotengwa Kagera kwaajili ya kukarabati wa miundombinu ya umeme na kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2018 miundombnu yote iwe imekarabatiwa.
“Kwa nchi nzima tuna umeme wa ziada megawati 209 isipokuwa changamoto kubwa sasa ni ubovu wa miundombinu kutokana na ukubwa wa nchi. Katika Mkoa wa Kagera tayari mradi umeme wa Rusumo ulionza kutekelezwa Februari 2017 unatarajia kukamilika Februari 2020 na utazalisha megawati 80 zitakazogawanywa katika nchi tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania na kila nchi itapata Megawati 26 na kuongeza umeme kwetu.” Alifafanua Waziri Kalemani
Aidha, Waziri Kalemani alisema kuwa tayari Mkoa wa Kagera umeunganishwa na Gridi ya Taifa ya Umeme kwa Wilaya ya Ngara na kufukia mwishoni mwa Mwaka huu 2018 Mkoa mzima utakuwa umeunganishwa na Gridi ya Taifa na umeme kutoka nchini Uganda utabaki kama wa ziada au Mkoa utaamua kuendelea au kutoendelea kutumia umeme huo.
Kuhusu umeme wa REA Waziri Kalemani alisema kuwa ziara yake Mkoani Kagera ililenga kutembelea baadhi ya vijiji katika Wilaya za Karagwe, Kyerwa na Missenyi ambapo miradi ya REA inatekelezwa ili kuona maendeleo ya mradi wa REA awamu ya tatu na kuona kama kuna changamoto ili ziweze kutatuliwa wananchi wapate umeme bila kucheleweshwa.
Waziri Kalemani alisema kuwa hadi kufikia mwaka 2021 Mkoa wa Kagera utakuwa umebakia na vijiji vichache sana ambavyo vitakuwa havijafikiwa na umeme. Aidha, aliendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia shilingi 27,000/= tu na si zaidi ya fedha hizo ili kuwekewa umeme wa REA. Pia aliwataka wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ili kuendelea kupata umeme bila hujuma.
Mwisho Waziri Kalemani aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha Taasisi zote za umma pamoja na maeneo yote yalipangwa kwaajili ya uwekezaji yanabainishwa na Wakandarasi waelekezwe kufikisha miundombinu ya umeme katika maeneo hayo. Taasisi za umma ni kama Shule, Zahanati, Makanisa, Misikiti, Maeneo yaliyotengwa kwaajili ya viwanda, Vyanzo vya maji vyenye miradi ya maji ya kutoa huduma ya kwa wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa