- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbalawa amewasili Mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 24 hadi 26 Machi, 2017 ambapo lengo la ziara yake likiwa ni kutembelea na kukagua Idara na Sekta zilizopo chini ya Wizara yake aidha, kukagua miundombinu na kuongea na watumishi katika idara na Sekta hizo juu ya mafanikio yaliyofikiwa na kutatua changamoto mbalimbali katika uboreshaji wa huduma.
Professa Mbalawa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bukoba alikagua uwanja huo na aliridhishwa na utendaji katika uwanja huo ambapo alisema kuwa kwasasa kuna mafanikio makubwa na kazi inafanyika kwa ufanisi mkubwa mara baada ya ujenzi wake kukamilika.
Pamoja na Professa Mbalawa kupongeza ufanisi wa kazi katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba aidha , Meneja wa uwanja huo Bi Dorice Uhagile katika taarifa yake kwa Waziri huyo alibainisha changamoto kubwa mbili ambazo ni uwanja huo kutokuwa na kituo cha kuongozea ndege (Contro Tower) . Pili ni Jengo la Watu Mashuhuri (VIP) kujengwa katika jengo la juu ghorofani badala ya majengo ya chini.
Akijibu changamoto hizo Professa Mbalawa alisema changamoto ambayo ataipa kipaumbele na kuishughulikia kwa haraka ni kuona uwezekano wa kujenga kituo cha kuongozea ndege kutokana na hali ya hewa ya Bukoba ili kulinda usalaama wa abiria wanaosafiri mara kwa mara kwa kutumia usafiri huo wa ndege.
Pia Professa Mbalawa alisema kuwa pamoja na changamoto hizo lakini yeye mwenyewe alijionea changamoto nyingine ambayo ni Shule ya Msingi Tumaini ambayo imejengwa karibu na uwanja huo jambo ambalo linahatarisha maisha ya wanafunzi pia na ndege wakati wa kuruka au kutua. Alisema kuwa uwanja huo una urefu wa kilometa 1.5 lakini unatakiwa kungezwa urefu kidogo kwajili ya usalama (buffer zone). Shule hiyo tayari inajengwa sehemu nyingine ili kupisha uwanja huo.
Katika hatua nyingine Professa Mbalawa alisema katika ziara yake atatembelea Bandari ya Bukoba na Kemondo ili kujionea miundombinu ya Bandari hizo. “Serikali ina mpango wa kununua meli ya kisasa ambayo itakuwa inatumika katika Ziwa Victoria kutoka Mwanza kuja Bukoba lakini lazima nijue kwanza miundombinu ya Bandari zetu isijekutokea kuwa Meli hiyo imefikishwa hapa halafu ikashindwa kufanya kazi kutokana na kutoendana na miundombinu ya bandari zetu kama kina cha maji au maegesho ya meli hiyo.” Alisistiza Professa Mbalawa
Tayari Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Professa Mbalawa ametembelea Uwanja wa Ndege wa Bukoba, TTCL, TEMESA na Shirika la Posta Kagera . Aidha atatembelea na kukagua Barabara ya Kyaka Bugene na Kivuko cha Kyenyabasa Wilayani Bukoba pia ataongea na wananchi ili kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na Wizara yake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa