- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Azindua Duka la Dawa Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera Agosti 17, 2017
Serikali Mkoani Kagera katika kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi imeanzisha na kuzindua duka la dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ili kuwahudumia wananchi waliokuwa wanaangaika kutafuta dawa nje ya Hospitali hiyo ambazo zilikuwa hazipatikani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Akizindua duka hilo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M.Kijuu Agosti 17, 2017 alitoa wito kwa viongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha duka hilo linaendeshwa kwa utaratibu mzuri na huduma nzuri zaidi. Aidha, kuhakikisha dawa zote za msingi zinapatikana na duka linatoa huduma masaa 24 kila siku.
Pia Mkuu wa Mkoa Kijuu aliusisitiza uongozi wa Hospitali hiyo kuwa na lengo la kupanua duka hilo ili litoe huduma kwa Zahanati na vituo vya afya katika Mkoa mzima. Yaani badala ya vituo hivyo kwenda kununua dawa, zinazokosekana Bohari ya Dawa (MSD), kwa maduka binafsi waje wanunue dawa hizo katika duka hilo.
Akitoa ufafanuzi Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa itaendelea kutoa huduma ya dawa katika dirisha lake la kawaida isipokuwa dawa ambazo zitakosekana katika dirisha la kawaida ndizo zitakuwa zinapatikana katika duka hilo kwa bei nafuu sana lakini siyo kwamba zitakuwa zinatolewa bure.
Duka hilo lilianza kufanyakazi tangu tarehe 01 Agosti, 2017 kama sehemu ya maandalizi na majaribio na kwa kipindi hicho, idadi ya wagonjwa wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwenda nje ya Hospitali hiyo kupata dawa imepungua. Duka hilo lilifanyiwa ukarabati kwa gharama ya shilingi milioni 22 na tayari dawa za kiasi cha shilingi milioni 30 zimenunuliwa kwa ajili ya huduma.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu alizindua Bodi ya Nne ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa baada ya Bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya ni Mzee Pius Ngeze ambaye ataongoza Bodi hiyo yenye wajumbe 15 kwa miaka mitatu.
Kwa kuboresha huduma na kuzisogeza karibu na wananchi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera inatarajia kuwaleta Madaktari Bingwa wa Magonjwa yote kuanzia tarehe 18 Septemba 2017 ambapo gharama za kuwaona Madaktari hao zitakuwa ni shilingi 5,000/= tu badala ya 25,000/= za kuwaona Madaktari bingwa katika Hospitali binafsi.
Akifafanua huduma hizo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dk. John Mwombeki Alisema wananchi watakaofanyiwa vipimo na kubainika kuwa watafanyiwa upasuaji watachangia gharama ya shilingi 30,000/= badala ya zaidi ya shilingi 500,000/= katika Hospitali binafsi. Huduma hizo hapo baadae zitalenga kufikishwa katika Halmashauri za Wilaya ili kuwafikia wananchi nwaliowengi zaidi vijijini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa