- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Jenga Uchumi na Redio Zetu Kagera “Redio Ni Wewe”
Tunapoelekea kuadhimisha Siku ya Redio Duniani Mkoa wa Kagera unajivunia kuwa na Vituo vya Redio Vipatavyo tisa sasa vinavyorusha matangazo yake ndani na nje ya Mkoa. Vituo hivyo vikiwa na malengo ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha wananchi vinarusha matangazo yake katika mfumo wa FM (Frequency Modulation) mfumo ambao unarusha mawimbi yake na kusikika vizuri kwa wananchi.
Kaulimbiu ya mwaka huu katika Maadhimisho Siku ya Redio Duniani Februari 13, 2018 inasema "Redio ni Wewe" ikilenga kuwa mifumo ya matangazo ya redio imebadilika kwa kuendana na teknolojia kiasi kwamba matangazo husikika hata kupitia simu za mkono, kwa hiyo mwananchi haitaji kubeba redio kubwa bali hata simu yake anaweza kusikiliza redio mahala popote atakapokuwa.
Mkoa wetu wa Kagera tunajivunia kuadhimisha siku hii muhimu sana kwani imekuwa ni hatua kubwa mkoa kuwa na vituo tisa sasa ambavyo vinarusha matangazo yake hapa mkoani. Vituo hivyo ni Kwizera FM, Kasibante FM, Vision FM, Karagwe FM, FADECO FM, Bukoba FM, Kagera Community Radio FM, Shinuz FM, na Mbiu FM (Ambayo ipo katika hatua za mwisho kuanza kurusha matangazo yake).
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu anasema haya ni mapinduzi makubwa katika Mkoa kuwa na vituo hivyo tisa vinavyorusha matangazo yake ndani na nje ya mkoa kwani vimekuwa chachu ya kuhamasisha maendeleo kwa wananchi, wananchi wenyewe hupata habari muhimu na kuelimika juu ya mambo mbalimbali kuhusu maendeleo yao.
“Sisi Serikali Redio hizi za kijamii zimetusaidia sana katika kuwapelekea wananchi jumbe mbalimbali hasa zinazohusu maendeleo ya mkoa katika kukuza uchumi. Lakini pia hata sisi viongozi wa Serikali hizi Redio zimetusaidia sana kujua kero mbalimbali za wananchi pale wanapopaza sauti zao kupiti redio hizo nasi kuzifanyia kazi mara moja. Kwahiyo unaweza kuona ni jinsi gani redio zetu zinavyoweza kutuunganisha na kuwa wamoja ,” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Kijuu.
Ikumbukwe kuwa hadi kufikia miaka ya 1990 Mkoa wa Kagera ulikuwa hauna kituo hata kimoja cha redio bali Redio zilizosikika wakati ule ni kutoka nje ya mkoa na zilikuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Redio Free Africa, Redio One, KBC (Kenya), Redio West (Uganda), na nyinginezo nyingi.
Mwaka 1995 ndipo Redio Kwizera ilianziashwa Wilayani Ngara lakini ikilenga kutoa habari zihusuzo Wakimbizi waliokuwa wamekimbilia Tanzania kutoka Rwanda na Burundi katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe. Baadae zilifuata Redio za Karagwe FM na FADECO FM mwaka 2007, Kasibante mwaka 2008 na nyinginezo zilifuata miaka ya 2010 hadi sasa.
Katika kuangalia utendaji na ufanisi wa Redio zetu za Mkoa wa Kagera mwanadisi wa makala haya aliongea na Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Kagera (KPC) Bw. Phinias Bashaya amabaye alisema kuwa Redio za Mkoa wa Kagera zimekuwa mkombozi kwa mwananchi wa kawaida tena wa kijijini kwani kupitia redio hizo wananchi wameweza kupaza sauti zao na wanasikika jambo ambalo hawakuwahi kulitarajia katika miaka ya 1990.
Bw. Bashaya Mwandishi Nguli anayeandikia Gazeti la Mwananchi alitoa ushari wake kwa Wamiliki wa Vituo vya Redio Mkoani kagera , Wahariri na Waandaji wa vipindi vya Redio kuzipa zaidi vipaumbele habari za wananchi ambapo alitoa mfano kuhusu Bomba la Mafuta linatoka nchini Uganda na kupita mkoani Kagera, kuwa wananchi wanatakiwa kuelimishwa juu ya fursa hiyo kupitia redio zetu za jamii.
“Tunapoadhimisha Siku ya Redio Duniani nawakumbusha wenzangu wandaaji wa vipindi kuangalia kwa jicho la tatu suala la utamaduni wetu, mfano naona redio zetu hazijajikita zaidi kuelimisha hasa vijana kuhusu utamaduni wa mwananchi wa Mkoa wa Kagera ili kulinda maadili ya Wanakagera. Mfano vijana wa leo wanatakiwa kujua wazee wetu walifanya nini wakati wa kuchumbia wake zao. Vipindi hivi ni vichache au wakati mwingine havisikiki kabisa, ningependa navyo vipewe kipaumbele pia,” Alisistiza Bw. Bashaya.
Aidha, Bw. Bashaya alitoa ushauri kuwa pamoja na Redioza Kagera kurusha vipindi vizuri lakini vituo hivyo vipunguze kurusha habari ambazo tayari zimerushwa na vyombo vya Kimataifa badala yake redio zetu zijikite katika habari za wananchi kwani Redio za kimataifa zinapenda kurusha habari mbaya tu lakini habari zetu nzuri hazirushwi kwahiyo redio zetu ziwe chachu ya kutangaza habari nzuri kwa wananchi wake.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Redio Kwizera FM Padri Damas Missanga aliwashauri wamiliki wa Vituo vya Redio Mkoani Kagera Kuhakikisha wanapata wawakilishi wa vituo vyao kila eneo ili kupata habari za wananchi. Alisistiza kuwa wananchi wanapenda kusikia habari zao wenyewe kuliko habari za kutokea sehemu nyingine.
Mwaka 2018 na Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi sasa inaendelea, tunaweza pia kutambua njia nyingi ambazo utangazaji wa michezo huleta watu pamoja, karibu na msisimko na mafanikio. Siku ya Radio Duniani, hebu tufurahie redio na michezo kama njia ya kuwasaidia watu kufikia mafanikio yao kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa