- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Serikali Mkoani Kagera Yapokea Vifaa vya Kisasa Kutekeleza Kwa Ufanisi Operesheni ya Kuondoa Mifugo na Wavamizi Kwenye Hifadhi
Serikali ya Mkoa wa Kagera imepatiwa vifaa vya kisasa ambavyo ni Ndege mbili zisizotumia Rubani (Drones) na Redio Upepo ishirini (Radio Calls) kwa ajili ya kufanikisha operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa misitu na mifugo inayochungiwa katika Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na Vyanzo vya maji ambapo uharibifu mkubwa ulikuwa unaendelea katika hifadhi hizo.
Makabidhiano ya vifaa hivyo yalifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera April 2, 2017 katika hafla fupi ambapo Simu 20 za upepo (Radio Calls) zenye thamani ya shilingi 25,000,000/= (Shilingi Milioni Ishirini na tano) zilitolewa na Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kutoka katika Kampuni yake binafsi ya SUN MACHNERY.
Pia Bw. Martine Loibook Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania alikabidhi ndege mbili zisizotumia rubani (Drones) zenye thamani ya dola 40,000 USD (Dola elfu arobaini) na kusema kuwa TAWA wamefurahishwa na jinsi Serikali ya Mkoa wa Kagera ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu inavyoendelea na zoezi la operesheni ili kunusuru Hifadhi za Misitu na Wanyamapori.
Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko naye pia alisema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha operesheni inafanikiwa kwa asilimia mia moja na vifaa hivyo vitasaidia kufanya operesheni kila eneo la Hifadhi la Mkoa wa Kagera bila kuacha wavamizi na mifugo katika maeneo hayo.
Kwaniaba ya Serikali Mkoani Kagera Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Deodatus Kinawilo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba alivipokea vifaa hivyo na alishukuru kwaniaba ya Serikali ya mkoa kuwa vifaa vilivyotolewa kuwa vitaongeza ufanisi katika operesheni hiyo. Aidha Kaimu Mkuu wa Mkoa aliendelea kutoa rai kuwa operesheni hiyo siyo nguvu ya soda bali maeneo yote ya hifadhi za Misitu na Wanyamapori yatasafishwa ili yabakie kama ilivyokuwa awali.
Aidha Bw. Faustine Masalu Mkurugenzi wa Huduma za Ulinzi na Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ambaye ni Mtekelezaji Mkuu wa Operesheni alisema operesheni inaendelea vizuri ambapo tayari watuhumiwa 19 na jumla ya mifugo 1922 ilikuwa imekamatwa kufikia April 2, 2017 Jumapili jioni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa