- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi mkakati wa kuimarisha usalama katika Mkoa wa Kagera uliopewa jina la “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama”. Mkakati huo ukilenga kuimarsha Ulinzi na Usalama wa mkoa kuanzia ngazi ya chini katika jamii kwa kila nyumba kumi kuwa na kiongozi ambaye atakuwa na jukumu la kutambua wanafamilia wanaoishi katika kila nyumba anayoiongoza.
Mkuu wa Mkoa Gaguti ambaye ni Mhasisi na Mwanzilishi wa Mkakati huo wa kukomesha uhalifu, ujambazi na vitendo vya uvunjifu wa amani katika Mkoa wa Kagera alizindua Mkakati huo kimkoa wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” wenye kaulimbiu isemayo: 10 Bora! Usalama wa Nchi, katika Kijiji cha Chabuhola Kata Nyakabanga Tarafa Nyakakika Wilayani Karagwe Novemba 1, 2018.
Akitoa ufafanuzi namna mkakati wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” utakavyofanya kazi Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaeleza wananchi waliofurika katika hafla fupi ya uzinduzi kijijini Chabuhora Wilayani Karagwe kuwa Mkoa wa Kagera bado haufanyi vizuri katika suala la ulinzi na usalama hasa watendaji wa Serikali katika ngazi za chini hawawajibiki ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao katika suala zima la kiulinzi.
“Katika Mkoa wetu wa Kagera bado tuna changamoto kubwa ya kiusalama hadi kufikia mwezi Septemba 2018 Mkoa ulikuwa na kesi za mauji 107, katika Kata hii tu tuliyopo hapa sasa ya Nyakabanga kufikia Septemba 2018 kulikuwa kumebainika wahamiaji haramu 997 na bado tunalo tatizo la magendo. Haya mambo makuu matatu yanonesha vyema kuwa bado tuna changamoto kubwa ya Kiusalama katika Mkoa”. Alieleza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa inashangaza sana kuona Mkoa wa Kagera wenye wasomi wengi na bado ni Mkoa unaoendelea kufanya vizuri katika Sekta Elimu lakini bado wananchi wake wanashiriki katika imani potofu na kupelekea kushiriki katika vitendo vya mauaji na kuifanya Kagera kuwa kati ya Mikoa ambayo inaongoza kwa vitendo vya mauaji.
Jukumu la Ulinzi na Usalama si jukumu la Vyombo vya Ulinzi na Usalama tu bali ni jukumu la kila mwananchi kulinda usalama wake mwenyewe na Usalama wa nchi na jukumu la Vyombo vya Ulinzi na Usalama ni kuongoza katika juhudi za kiulinzi na kiusalama pale panapotokea uvunjifu wa amani. Mwananchi mmoja mmoja anatakiwa kulinda usalama popote pale anapokuwa katika nchi ya Tanzania.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Mkoa wa Kagera unatakiwa kuwa mbele sana katika suala la kiusalama kwani unapakana na nchi jirani nne kati ya nchi nane zinazopakana na nchi ya Tanzania. “Mtu akiingilia hapa Nyakabanga anajifanya mwenyeji na mwisho wa siku anatupigia bao Dodoma katikati ya nchi akishafika huko anajifanya ametokea Chabuhora Nyakabanga Karagwe kumbe mhamiaji Haramu.” Alifafanua Mhe. Gaguti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bw. Godfrey Mheluka akito taarifa kwa Mkuu wa Mkoa alisema baada ya Wilaya ya Karagwe kupewa heshima ya kuzindua Mkakati wa “Nyumba Kumi Bora za Kiusalama” uongozi wa Wilaya uliamua kufanya uzinduzi huo katika Kata ya Nyakabanga kwasababu kata hiyo inaongoza kwa mauaji na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na mkakati huo ulizinduliwa hapo kuanza kukomesha vitendo hivyo.
Namna Mkakati wa Nyumba Kumi Bora za Usalama Utakavyofanya Kazi.
Kila Kijiji zinatengwa nyumba kumi kumi na kila nyumba kumi anachaguliwa kiongozi mmoja ambaye anajua kusoma na kuadika. Kila nyumba au kaya wanaorodheshwa wanafamilia wanaoishi katika nyumba hiyo na kunakuwa na orodha ya kila nyumba kwa nyumba zote kumi.
Majukumu ya Kiongozi ni kuhakikisha katika nyumba zake kumi hakuna mgeni anayeingia au kuishi bila kuwa na taarifa za mtu huyo ametokea wapi au amekuja kufanya nini katika eneo hilo. Jukumu la mwananchi ni kutoa taarifa kwa Kiongozi wa Nyumba Kumi za Kiusalama apatapo wageni na taarifa za muhimu za mgeni huyo ili kuzuia uvunjaji wa amani kwa watu wasiojulikana wanatokea wapi au wamekuja kufanya nini.
Aidha, katika kuzuia wizi wa mifugo wananchi watatakiwa kutoa taarifa kwa Kiongozi wao pale wanapotaka kuchinja mbuzi au ngombe kwaajili ya kuuza au kitoweo cha nyumbani katika familia zao ili Kiongozi ahahkikishe kuwa mnyama huyo si wa wizi
Viongozi wa Nyumba Kumi za Kiusalama wanapewa mihuli iliyo na namba ziatakazotofautisha Vijiji na Kata ambapo wataruhusiwa kuandika barua za kuwatambua wakazi wao na kuwatolea taarifa mbalimbali kwa viongozi wao wa juu. Wasimamizi wakuu wa viongozi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama ni Watendaji wa Vijiji pamoja na Watendaji wa Kata.
Kila Nyumba Kumi za KIusalama wananchi na kiongozi wao watatakiwa kufanya mikutano ya kujadili ulinzi na usalama kila mwezi na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwa mtendaji wa Kijiji ambapo naye ataunganisha taarifa hizo na kuziwasilisha kwa Afisa Mtendaji wa Kata. Taarifa hizo zitaenda mpaka ngazi ya Wilaya hadi Mkoa ili kama kuna changamoto kubwa ya kiusalama ifanyiwe kazi kwa wakati.
Katika hafla hiyo fupi ya uzinduzi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama zilitolewa mada kuhusu Urai kutoka Ofisi ya Kamanda wa Uhamiaji Mkoa, Usalama wa Raia kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera . Aidha, uzinduzi huo ulihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera. Kuwa kiongozi wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama si ajira ya kulipwa mshahara wala posho bali ni uzalendo wa mwananchi mwenyewe kushiriki katika kulinda usalama wan chi.
Nao wananchi wa Kata ya Nyakabanga walifurahi na kupokea mkakati huo kwa mikono miwili ambapo walisema kuwa sasa huo unakwenda kuwa mwarobaini wa kukomesha uhalifu, mauaji na magendo. “Wahamiaji haramu wanakuja hapa wanafanya matendo maovu kama mauaji alafu tunaonekana ni sisi wakazi wa hapa kumbe siyo sasa huu mpango wa Nyumba Kumi Bora za Kiusalama utatusaidia sana katika kuwatambua haraka na tunamshukuru Mkuu wa Mkoa.” Alieleza Bw. Amosi Balikweba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa