- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Akagua Miradi ya Afya Kuona Shilingi Bilioni 3.5 Fedha za Serikali Zinatumika Kama Ilivyokusudiwa
Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu afanya ziara katika Halmashauri za Wilaya nane kukagua matumizi ya shilingi bilioni 3.5 fedha zilizotolewa na Serikali kukarabati baadhi ya Vituo vya Afya Mkoani Kagera pia kuwahamasisha wananchi kuendelea kuchangia gharama za ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya ambavyo havijakamilika katika maeneo yao kwa kushirikiana na Serikali.
Akiongea na wananchi katika Kituo cha Afya Nyakanazi Wilayani Biharamulo Mkuu wa Mkoa Kijuu alisema kuwa alifika kituoni hapo pamoja na Vituo vingine vya Afya ambavyo vimepewa fedha na Serikali ili vikarabatiwe ili ajionee kama fedha hizo zinatumika ipasavyo ikiwa ni pamoja na michango ya wananchi wa eneo husika na kuhakikisha ujenzi unakamilika ifikapo Machi 30, 2018.
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kwa vituo vinane katika Mkoa wa Kagera ambapo awamu ya kwanza ilitolewa shilingi milioni 500 kwa kila kituo Vituo vya Nyakanazi (Biharamulo) na Kayanga (Karagwe). Awamu ya pili Serikali ilitoa shilingi milioni 500 kituo cha Katoro (Bukoba) na Vituo vya Kishanje (Bukoba), Mabawe na Murusagamba (Ngara), Kimea (Muleba), na Murongo (Kyerwa) vilipewa shilingi milioni 400 kila kimoja.
Akitoa ufafanuzi Mkuu wa Mkoa Kijuu kwenye Mikutano ya hadhara na wananchi alipotembelea na kukagua ukarabati wa Vituo vilivyopata fedha kutoka Serikalini alisema kuwa Vituo hivyo vilipata fedha katika awamu ya kwanza kutokana na juhudi za wananchi wenyewe katika maeneo husika kuonesha juhudi katika uchangiaji wa ujenzi wa Vituo vyao vya Afya.
Mkuu wa Mkoa Kijuu aliwahamasisha wananchi katika maeneo mengine ambayo vituo vyao havijapata fedha kutoka Serikalini kuendelea kuchaangia ujenzi wa Vituo na Zahanati ili majengo na miundombinu yote inayotakiwa ikamilike, kupitia juhudi hizo za wananchi Serikali pia itaweza kuchangia fedha kwa maeneo yale ambayo wananchi wataonesha juhudi za kuchangia maendeleo yao.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alisistiza mambo makuu manne kama ifuatavyo, Kwanza, Vituo vya Afya vilivyopata fedha za Serikali zitumike kwa kusimamiwa na Kamati za Vituo pia watumike mafundi wa eneo husika bila kuwatumia Wakandarasi na Wakandarasi washauri katika ujenzi ili kuepuka gharama kubwa za ujenzi aidha, ujezi uzingatie viwango kwa usimamizi wa Wahandisi wa Halmashauri.
Pili, Mkuu wa Mkoa aliwaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kuhakikisha wanatenga na kuyapima maeneo ya Vituo vya Afya na Zahanati kwa manufaa ya upanuzi wa baadae na kuondoa migogoro na wananchi jirani. Tatu, wananchi wanatakiwa kuendelea kujishughulisha na kilimo ili kujipatia chakutosha na kuchangia maendeleo yao kama ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya.
Nne, wananchi, Taasisi za Serikali na zisizokuwa za Serikali zinatakiwa kupanda miti ya matunda kuzunguka maeneo ya Taasisi hizo na wananchi wapande miti ya matunda ya aina mbalimbali isiyopungua mitano kuzunguka kaya zao ili kupunguza tatizo la utapiamlo katika Mkoa wa Kagera ambalo linatokana na wananchi wa Kagera kutokula matunda na mchanganyiko sahihi wa vyakula.
Katika hatua nyingine kwenye ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas Rutachunzibwa ambaye alipata fursa ya kuwaelimisha wananchi juu ya miundombinu inayotakiwa katika Vituo vya Afya na Zahanati ambapo ili kituo cha Afya kiitwe Kituo cha Afya kinatakiwa kuwa na miundombinu ifuatayo:
Kituo cha Afya kilichokamilika na kuruhusiwa kutoa huduma kwa wananchi kinatakiwa kuwa na Jengo la Wagonjwa nje na wagonjwa wa ndani, Jengo la Maabara, Wodi ya akinamama, Jengo la upasuaji, Wodi nyingine za wagonjwa, Vyoo vya watumishi na wagonjwa, Nyumba za watumishi wawili, Kichomea taka, Maji ya kutosha, Nishati ya umeme na Nyumba ya kuhifadhia maiti.
Dk. Rutachunzibwa aliwakumbusha wananchi katika ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa kuwa kwa sasa Serikali imetoa ramani ya ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati ambapo wananchi wanatakiwa kuzingatia ramani hizo wakati wa ujenzi ili majengo ya kutolea huduma za afya yakidhi viwango.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa