- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kaya Elfu Tano za Kagera Kunufaika na Mradi wa Kilimo na Ufugaji Ili Kurejesha Hali zao Katika Maisha ya Kawaida Baada ya Tetemeko
Kaya elfu tano (5000) za wananchi wa Mkoa wa Kagera zilizoathirika na Tetemeko la ardhi lililotokea mwaka jana Septemba 10, 2016 zatarajia kunufaika na mradi wa miaka miwili wenye thamani ya zaidi shilingi milioni 600 kupitia kilimo na ufugaji chini ya ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Mradi huo wa kurejesha hali za wananchi baada ya tetemeko chini ya ufadhili wa (FAO) ulizinduliwa rasmi Mkoani Kagera Mei 5, 2017 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu pamoja na Mwakilishi wa (FAO) nchini Tanzania Bw. Fred Kafeero ikiwemo na wadau ambako mradi utatekelezwa.
Malengo ya mradi ni kuvisaidia vikundi vya wakulima hasa vijana na akina mama kupitia mfumo wa mashamba darasa na stadi za maisha. Kuwajengea uwezo wa matumizi ya mbinu na teknolojia zinazokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao kwa kulinda rasilimali ardhi na misitu.
Aidha, kuimarisha kilimo kinachozingatia lishe bora ili kupunguza utapiamlo hasa kwa wtoto wadogo na kuwaelimisha wakulima na wafugaji namna bora ya kupata masoko ya mazao yao ili kujiongezea kipato.
Mwakilishi wa (FAO) nchini Tanzania Bw. Fred Kafeero alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa kutumia raslimali zilizopo siyo kwamba utatekelezwa kama mradi mpya. “Tunalenga kutumia raslimali na njia ambazo tayari zilikuwepo awali mfano kutumia vikundi vya vijana na wakulima au wafugaji ambao tayari wapo ili kutekeleza mradi huu.” Alisistiza Bw. Kafeero
Bw. Kafeero alisema kuwa mradi huo umekuja Kagera baada ya yeye kutembelea mkoani hapa mwaka jana Oktoba 16, 2017 akiwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charles Tizeba na kujionea hali ya ukame wa muda mrefu na madhara ya tetemeko jinsi vilivyoathiri uzalishaji wa chakula hasa zao la ndizi na kupelekea wananchi kukosa chakula na kipato kutokana na kutopata mavuno ya kutosha.
Katika ripoti ya utafiti wa Afya ya mwaka 2015/16 mkoa wa Kagera ulikuwa na asilimia 41.7% ya udumavu na kiwango kikubwa cha upungufu wa damu mwilini kwa watoto asilimia 39.1% na akinamama asilimia 57.2% jambo ambalo lilionekana kuathiri matumizi ya lishe bora kwa ngazi ya kaya na kupelekea utapiamlo kwa watoto. Pia majanga ya asili na ukosefu wa ujuzi katika kilimo kwa wakulima wadogo ni changamoto kubwa katika uzalishaji wa chakula na lishe bora kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu alilishukuru Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO)kupitia mwakilishi wake nchini Bw. Fred Kafeero kuleta mradi huo kwa wananchi wa Kagera hasa baada ya kupata majanga ya ukame na tetemeko. “Kwaniaba ya wananchi wangu nawashukuru sana kwani mradi huu utakuwa faraja kwa wananchi hasa baada ya kupata majanga ya asili.” Alisistiza Mhe. Kijuu.
Mkuu huyo wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwaagiza Watendaji na watekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wantekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa ambapo alisema kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi lakini mwisho wa miradi hiyo hakuna tija kama inavyokuwa imetarajiwa hapo awali. Alisistiza kuona matokeo mazuri katika jamii na wananchi wenyewe mradi utakakokuwa unatekelezwa.
Mradi wa kurejesha hali za wananchi baada ya Tetemeko Kagera ambao utafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) utatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za tano ambazo ni Muleba, Kyerwa, Missenyi, Bukoba na Bukoba Manispaa.
Watekelezaji wakuu wa mradi huo ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama mtekelezaji mkuu wa mradi kwaniaba ya Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kama msimamizi wa karibu wa mradi, Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) wafadhili wa mradi, na Halimashauri za Wilaya ambazo ndiyo wanaohusika moja kwa moja katika kutekeleza mradi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa