- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Luaga Mpina Ahamasisha Wafugaji Kagera Ng’ombe Wao Kupigwa Chapa Kukomesha Uingizwaji wa Mifugo Toka Nje.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luaga Mpina afanya ziara ya siku mbili Mkoani Kagera kuhamasisha kasi ya upigaji chapa wa ng’ombe ili kutambua idadi ya mifugo hiyo ikiwa ni pamoja na kukomesha wizi wa ng’ombe pia na kukomesha uingizwaji wa ng’ombe hao nchini kutoka nchi za jirani.
Akiwa Mkoani hapa Waziri Mpina alishiriki katika zoezi la kupiga chapa ng’ombe katika Wilaya ya Bukoba Kijijini Kyema Kata Katerero ambapo mara baada ya kushiriki zoezi hilo akiongea na wafugaji walioleta ng’ombe wao kupigwa chapa katika zoezi hilo alisema,
“Lengo kuu la kupiga chapa ng’ombe ni kuzuia wizi wa ng’ombe, kupata takwimu halisi za ng’ombe nchini ili kuisaidia Serikali kuweka mipango sahihi ya uendelezaji wa ufugaji nchini. Lakini pia kuhakikisha ng’ombe wa Tanzania wanakuwa na alama ambapo itasaidia kutambua ng’ombe kutoka nchi jirani wanaoingizwa kulishwa nchini kwetu. Aidha zoezi la kupiga chapa ng’ombe ni la nchi nzima ambapo mwisho wa zoezi hilo utakuwa tarehe 31.12.2017” Alisistiza Waziri Mpina.
Pia Waziri Mpina akiwa Mkoani Kagera alizitembelea Ranchi za Missenyi na Pori la Akiba la Burigi na kujionea jinsi mifugo kutoka nchi jirani ilivyoondolewa kutoka katika mapori hayo. Pia alishuhudia ng’ombe zaidi ya 6000 walioingizwa katika mapori hayo kutoka nchi jirani waliokatawa mara baada ya Operesheni Ondoa Mifugo Kagera na kuagiza ng’ombe hao kupigwa mnada mara moja.
Waziri Luaga mpina katika ziara yake ya siku mbili Kagera alitembelea pia kiwanda cha kusindika minofu ya Samaki cha SUPREME PERCH kilichopo eneo la Nyamkazi Manispaa ya Bukoba ambapo uongozi wa kiwanda hicho ukitoa taarifa ulisema kuwa hadi sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika tani 60 za minofu ya samaki lakinikwasasa kinasindika tani 17 tu kutokana na uhaba wa Samaki.
Mara baada ya kupokea taarifa hiyo Waziri Mpina aliuagiza uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha ndani ya mwaka mmoja ujao kiwe kimefikia angalau uzalishaji wa tani 25 na kufikia mwaka 2020 kizalishe tani zote 60 kwani Serikali inakwenda kuhakikisha inakomesha vitendo vyote vya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.
Vilevile Waziri mpina alitembelea shamba la mabwawa ya kufuga samaki katika eneo la Luhanga Wilayani Muleba na kujionea ufugaji wa samaki wa kisasa na ambapo alisema kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi kufuga samaki katika mabwawa ili kutoa nafasi ya kupumzisha ziwa ili samaki wazaliane kwa wingi.
Mwisho Waziri Luaga Mpina aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kufanya operesheni ondoa mifugo Kagera na kuhakikisha Ng’ombe wote kutoka nje ya nchi wameondolewa katika Mapori ya Akiba na hifadhi za Taifa. Waziri Mpina alifanya ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 1 hadi 2 Novenba, 2017 na kumalizia ziara yake Wilayani Biharamulo ambapo aliondoka kuelekea Mkoani Kigoma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa