- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkoa wa Kagera katika kuadhimisha kilele cha wiki ya Sheria Februari 6, 2019 Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Bukoba chini ya Jaji Mfawidhi Lameck M. Mlacha imeweza kusikiliza kwa mara ya kwanza kesi Namba 56 ya mwaka 2018 ya Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira na Mwalimu Erieth Gerald dhidi ya mauaji ya Mwanafunzi marehemu Spelius Eradius wa Kibeta Shule ya Msingi Manispaa ya Bukoba aliyepigwa hadi kupelekea mauti ya kifo chake tarehe 27.08.2018
Katika shauri hilo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Msomi Chema Maswi Kaimu Mwendesha Mashitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo aliwasilisha mashahidi saba kutoa ushahidi katika shauri hilo. Shahidi wa kwanza Bw. Benius Benezeth ambaye ni dereva bodaboda aliyembeba Mwalimu Erieth Gerald siku ya tukio alitoa ushahidi mbele ya Mahakama jinsi alivyombeba mwalimu huyo na kumfikisha shuleni Kibeta na kupokelewa mizigo na wanafunzi.
Baada ya kutoa ushahidi mbele ya Mahakama shahidi wa kwanza Bw. Benius Benezeth na kuhojiwa na pande zote mbili upande wa Jamhuri na upande wa utetezi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Lameck M. Mlacha alihairisha kesi hiyo hadi tarehe 8.02.2019 ambapo mashahidi wengine sita wataendelea kutoa ushahidi wao mbele ya Mahakama.
Kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2018 ilisikilizwa mara baada ya hafla fupi ya ufunguzi wa mwaka mpya wa shuguli za Mahakama kumalizika katika viwanja vya Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Bukoba ambapo wananchi na wageni waalikwa waliruhusiwa kuhudhuria na kusikiliza kikao hicho cha Mahakama Kuu kilichoashiria kuwa sasa shughuli za Mahakama Mkoani Kagera zimefunguliwa rasmi.
Kabla ya kikao hicho cha Mahakama Kuu Jaji Mfawidhi Lameck M. Mlacha akitoa hotuba yake mbele ya wageni waalikwa alisema kuwa maana ya kuadhimisha kilele cha maadhimisho ya wiki ya Sheria kwanza ni kiashiria cha kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama, Pili ni kuomba dua ili haki itendeke kwa wananchi Mahakamani, na tatu ni kufanya tathimini ya utendajikazi wa Mahakama kwa kipindi kilichopita na kujisahihisha.
Akiwapongeza baadhi ya wadau wa Mahakama Jaji Mfawidhi Lameck M. Mlacha alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati akitolea mfano wa upelelezi wa kesi ya mauaji ya Mwanafunzi Marehemu Spelius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta aliyefikwa na Mauti baada ya kupigwa na Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira kufanyika kwa weledi na kwa wakati jambo ambalo lilipelekea kesi kufikishwa mahakani kwa wakati.
Onyo, Jaji Mfawidhi Mlacha alitoa onyo kwa baadhi ya Mahakimu Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi, na baadhi ya Makarani katika Mahakama ambao bado wanajihusisha na kupokea au kushawishi kupewa rushwa kuwa wakigundulika watachukuliwa hatua kali kwani zama hizi si zile walizozizoea vinginevyo wabadili mienendo ya tabia hizo mara moja na kutenda haki kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akitoa salamu za Serikali katika hafla hiyo aliipongeza Mahakama kwa kudumisha utamaduni wa kuadhimisha Wiki ya Sheria tena kwa kutoa msaada wa kisheria na elimu kwa wananchi na baadhi ya makundi mbalimbali ili yaweze kuelewa vizuri namna ya kutafuta haki Mahakamani.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama kupitia vyombo mbalimbali ambavyo vipo chini ya Serikali kukomesha Wanasheria na Mawakili Vishoka wanaowarubuni wananchi na kufanya kazi za kisheria bila weledi wa kutosha na kuwafanya wananchi kuendelea kupoteza muda mwingi Mahakani bila sababu.
“Kila mmoja hapa anajua kuwa Mkoa wa Kagera una wasomi wengi hasa Maprofesa lakini nasikitika sana kusema kuwa wakati mwingine wasomi hao wamekuwa kichocheo cha wananchi kushinda Mahakamani wakati mwingine hata kama mwananchi huyo hana haki lakini analazimika kuendelea kufuatilia kesi kisa tu ana ndugu ambaye ni Profesa.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Aidha Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa onyo kwa wananchi wanaojichukulia sheria mikononi katika Mkoa wa Kagera kuacha tabia hiyo kwani vitendo hivyo vinaupa mkoa sifa mbaya kama ilivyokuwa katika ujambazi wa kutumia siraha. Alisisitiza kuwa hapo nyuma Mkoa wa Kagera ulisifika kwa matendo ya ujambazi lakini Serikali ilikomesha vitendo hivyo na sasa Kagera ipo katika mikoa inayofanya vibaya katika kujichukulia sheria mikononi.
Akihitimisha Salamu za Serikali Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaomba Viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, uvumilivu na upendo kwa waamini wa madhehebu yote ili wananchi waache vitendo viovu na kumrudia Mwenyezi Mungu jambo ambalo litapunguza kesi Mahakamani na kuwafanya wananchi kutumia muda mwingi kuzalisha na kufanya kazi za kujiingizia kipato.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa