- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mradi wa Uimarishaji Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST Dialogue) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chemba ya Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) waendesha mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi katika Mkoa wa Kagera ili kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara kwa ushirikiano wa Serikali na Wadau wa biashara.
Mafunzo hayo kwa kiasi kikubwa yalilenga hasa kujadili kwa pamoja namna nzuri ya kuweka Mazingira bora ya Biashara na Ushawishi wa Sekta Binafsi katika kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla ili lengo la maendeleo liweze kufikiwa kwa pamoja.
Katika mafunzo hayo Viongozi wa Serikali pamoja na Wadau mbalimbali walifundishwa juu ya mfumo wa ushawishi na majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ambapo sekta hizo mbili zilikumbushwa kushirikiana na kujadiliana mara kwa mara katika kuhakikisha biashara zinafanyika vizuri katika mazingira wezeshi.
Akiwasilisha mada ya kuweka mazingira mazuri ya biashara Dkt. Swabiri Khalid kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa Sekta ya Umma inatakiwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ili Sekta binafsi waweze kufanya biashara zao bila wasiwasi pia kama kuna changamoto zozote katika sekta hizo mbili ni vyema kukaa pamoja na kuzitatua changamoto hizo kwa pamaoja na uelewa wa mmoja.
Sekta ya Umma ambao ni Viogozi mbalimbali wa Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi katika mafunzo hayo walibainisha changamoto mbalimbali za kila Wilaya katika mkoa wa Kagera zinazokwamisha au kuweka mazingia yasiyokuwa rafiki katika biashara na kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo ili kuweka mazingira rafiki ya biashara.
Changamoto kubwa zilizobainishwa katika mafunzo hayo ni Sekta binafsi kuiona Sekta ya Umma kama adui yake badala ya kuiona rafiki na kushirikiana. Pili Wadau wa Sekta Binafsi walilalamikia kodi kuwa nyingi lakini Sekta ya Umma nao walilalamikia ukwepaji wa kodi kwa wafanyabiashara. Tatu, wafanyabiashara kutopendana na kushirikiana katika kutafuta fursa za biashara. Nne, migogoro mingi ya ardhi.
Katika kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo Sekta hizo mbili za Umma na Binafsi zinatakiwa kushirikiana kwa kufanya mikutano ya pamoja na kutafuta njia mbadala ya kutatua tatizo. Aidha, elimu kwa wafanyabiashara inatakiwa kutolewa ili waelimishwe juu ya biashara zao, fursa mpya pamoja na umuhimu wa kulipa kodi za Serikali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. CP Diwani Athuman akitoa rai katika mafunzo hayo aliwaasa washiriki wa mafunzo, watumishi wa umma na wafanyabiashara Mkoani Kagera kubadilika kimtazamo ili kuchangamkia fursa nyingi zilizopo. Pili CP Athumani alisisitiza kuzitangaza fursa za uwekezeji katika mkoa kwa nguvu zote hasa kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo Tovuti ya Mkoa na Halmashauri za Wilaya .
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu akifunga mafunzo hayo aliishukuru Taasisi ya BEST Dialogue kwa kuwezesha mafunzo kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na kusema kuwa mafunzo hayo yalichelewa sana kama yangelifanyika miaka miwili nyuma mkoa ungekuwa mbali kimaendeleo kwani wafanyabiashara wangekuwa wamechangamkia fursa bila vikwazo.
Mkuu wa Mkoa Kijuu aliziagiza Halmashauri zote za Wilaya Mkoani Kagera kufanya vikao vya kubainisha changamoto zinazoweka mkwamo wa mazingira mazuri ya biashara na kuzitafutia ufumbuzi Sekta ya Umma kwa kushirikiana na Sekta binafsi ili kuwa na uelewa wa pamoja.
Pia aliwaagiza viongozi Chemba ya Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Kagera kuandaa kikao cha wafanyabiashara Mkoani Kagera pamoja na Serikali ili kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha biashara mkoani hapa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa