- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kaasim Majaliwa katika siku yake ya tatu akiwa ziarani Mkoani Kagera katika Wilaya ya Biharamulo Oktoba 8, 2018 aongea na watumishi wa umma na kuwakumbusha wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi na kutoa msimamo wa Serikali katika utendaji kazi wa Watumishi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na watumishi wa umma Wilayani humo aliwakumbusha watumishi wa umma kuwa wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa matakwa ya Serikali na Kiongozi aliyepo madarakani na kusisitiza kuwa matakwa ya Serikali ya Awamu hii ya Tano ni Hapa Kazi Tu na kila mtumishi anatakiwa kuchapa kazi kwa bidii, kuwa na mpango kazi wa kazi zake na kufanya tathimini ya kazi zake anazozifanya kama zina tija kwa Wananchi.
“Mwananchi anatakiwa kupokelewa, kusikilizwa na kuhudumiwa na Watumishi wa Serikali za Mitaa mnatakiwa kukaa ofisini siku moja na kutumia siku nne kwenda vijijini kuwahudumia wananchi. Wakuu wa Wilaya ambao ndiyo Wakuu wa Shughuli za Serikali Wilayani mnatakiwa kuwasimamia Wakuu wa Idara kuhakikisha wanaenda vijijini kuwahudumia wananchi.” Alisistiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasistiza watumishi kuwa wanatakiwa kuwahudumia wananchi bila kuwabagua kwa njia yoyote ile iwe siasa au kabila ambapo lengo kuu la Serikali likiwa ni kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi hao na watumishi ambao hawatawajibika watachukuliwa hatua kulingana na Sheria, kanuni na taratibu.
Ukusanyaji wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Serikali Yasiyoridhisha - Biharamulo
Katika utangulizi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akimkaribisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuongea na watumishi alisema kuwa yeye kama Mkuu wa Mkoa haridhishwi na ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha zinazokusanywa na Halmashauri ya Biharamulo na alichukua hatua za kwa kuwachunguza watumishi saba na wawili kati ya hao kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi kwa kumagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua.
Akiongelea suala hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Halmashauri za Wilaya zina vyanzo vya mapato viwili, kwanza Mapato ya ndani ambayo yanakusanywa na Halmashauri inatumia fedha hizo katika kusaidia kujazia penye upungufu pale wananchi wanapokuwa wametekeleza mradi na wananhitaji msaada wa Serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisisitiza kuwa fedha za Serikali za mapato ya ndani katika Halmasauri za Wilaya zinatakiwa kukusanywa kwa mashine za kielektroniki sehemu zote za vyanzo vya kukusanyia mapato. Aidha, watumishi katika Halmashauri wanatakiwa kubuni vyanzo vya mapato na kukusanya mapato hayo na kwa watumishi wanaotakiwa kukusanya lakini hawakusanyi Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya waliagiza kuwachukua hatua za kisheria.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa angalizo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na vita kali ya kupambana na Rushwa kwa hiyo watumishi wanatakiwa kutojihusisha na Rushwa na alimkumbusha Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kuwa wameagizwa kuhakikisha wanafanya kazi kila sehemu ili kubaini wala rushwa. Serikali hivi karibuni inatarajia kufanya marekebisho ya Sheria ili Makamanda wa TAKUKURU Mikoa waweze kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani badala ya Makao Makuu tu.
Maagizo ya Waziri Mkuu Katika Utoaji wa Huduma za Kijamii Kwa Wananchi Wilayani Biharamulo
ELIMU, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aligiza Idara ya Elimu Wilayani Biharamulo kuhakikisha shule zinagawiwa vitabu na vinatumika kwa wanafunzi kuvisoma ili viwasaidie na si kuvibakiza vitabu hivyo katika makabati tu. Pili, Kuongeza Shule za Kidato cha Tano kama kuna sehemu ina uhitaji wa shule hizo. Nne, kudhibiti tatizo la Mimba za utotoni kuanzia Shule za Msingi hadi Kidato cha Sita na atakayebainika sheria itachukua mkondo wake na adhabu ni miaka 30 Jera.
MAJI, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza Waandisi kuhakikisha kuwa wanapotekeleza miradi ya maji wahakikishe pale panapotakiwa kuchimbwa kisima cha maji pawe pamepimwa na kuwa na uhakika wa maji kupatikana hapo na siyo kuchimba tu na mwisho ndiyo inagunduika kuwa hakuna maji wakati fedha za Serkali zimeishatumika.
AFYA, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa aliwaagiza Watendaji wa Halmashauri ya Biharamulo kuahakikisha wanawahamasisha wananchi kujenga maboma ya Zahanati katika vijiji na Halmashauri kutoa bati ili kumalizia Zahanati hizo. Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali Kuu imejikita katika kuboresha huduma za Afya kwa kuboresha na kujenga vituo vya Afya na tayari Biharamulo wamepata Shilingi Milioni 100 kwa ajili kujenga na kuboresha Vituo vya Afya viwili.
Vilevile Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa alihaidi kuwa Wilaya ya Biharamulo kwa kuwa haina Hospitali ya Wilaya Serikali itatoa shilingi bilioni 1.5 katika awamu ya pili ili Hospitali ya Wilaya iweze kujengwa. Mganga Mkuu wa Wilaya aliagizwa kuhakikisha anasimamia mgawanyo wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za Afya na kuwaelimisha wananchi ni dawa zipi zinatakiwa kupatikana katika kila ngazi ya kituo cha kutolea huduma za afya (Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali na Hospitali za Rufaa)
MIUNDOMBINU, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara za Vijijini zinapitika kwa wakati wote wa masika na kiangazi na kuendelea kujenga barabara za mijini kwa kiwango cha rami ili kuboresha maeneo ya miji.
NISHATI YA UMEME, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imesambaza umeme hadi vijijini ili kutatua tatizo la uharibifu wa mazingira na kumuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilayani Biharamulo kusimamia kikamilifu na kuhakikisha kila mwanachi anapata umeme katika nyumba yake kwa gharama ya shilingi 27,000/= tu.
KILIMO, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza Maafisa Kilimo kutoa elimu kwa wananchi ili walime na kuzalisha kwa tija mazao ya chakula na biashara katika maeneo madogo. Aidha, Waziri Mkuu alimuuliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo Bi Wende Ng’ahala kama agizo lake lilitekelezwa la kuwahamishia Maafisa Kilimo wote vijijini kuwasaidia wananchi ambapo Bi Wende alijibu kuwa agizo hilo halijatekelezwa.
Mkurugezi aliulizwa kuwa anao Maafisa wangapi wa Idara ya Kilimo Ofisini kwake ambapo allijibu kuwa anao Maafisa Wanne na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka Maafisa hao kusimama ndani ya ukumbi na kumwagiza Mkurugenzi kuondoka kwenye kikao kwenda kuwaandikia barua za kuhamia vijijini kuwasaidia wananchi katika masuala ya kilimo Maafisa wawili na kubakiza wawili Makao makuu ya Halmashauri.
Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Biharamulo Bi Wende alitekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kwa kuwaandikia barua za uhamisho Maafisa wawili waIdara ya Kilimo ambapo Bw. Juma M. Deja Afisa Kilimo II alihamishishwa kuhudumia Kata ya Nyakatahoka na Nyarubungo, aidha Bw. Bruno Ngawagala Afisa Kilimo Msaidizi Mkuu Ialihamishwa kuhudumia Kata za Bisibo na Nyakiziba.
ARDHI, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuweka vigingi vinavyoonekana katika mapori ya Biraharamulo, Burigi na Kimisi (BBK) ili kuondoa migogoro ya ardhi kati ya Shirika hilo na wananchi. Aidha, alimwagiza Meneja wa Mapori ya (BBK) Kagoma Bigiramungu kumrejesha Mhasibu Adamu katika majukumu yake ya Kihasibu na kumuondoa mara moja Bi Ruth Mhifadhi Wanyamapori katika majukumu ya kihasibu na kumrejesha katika majukumu ya taaluma yake aliyoisomea.
Mwisho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Biharamulo kuimarisha ulinzi na Usalama kwani Wilaya hiyo inapakana na nchi jirani na kuruhusu wahamiaji haramu kuingia bila kufuata taratibu kanuni na sheria za nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa