- Mwanzo
- Kuhusu Sisi
- Utawala
- Wilaya
- Halmashauri
- Fursa za Uwekezaji
- Huduma
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako afanya ziara ya siku moja Kagera na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mkoani Kagera ili kuona ni hatua gani imefikiwa katika ujenzi huo ili vianze au viendelee kutoa huduma fanisi kwa wananfunzi wanaohitimu Elimu ya Msingi na Kidato cha nne.
Profesa Ndalichako akiwa Mkoani Kagera Januari 26, 2019 alitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Kagera katika Kijiji cha Burugo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kilometa chache kutoka Bukoba Mjini.
Profesa Ndalichako alitembelea Burugo kwenda kujihakikishia kama jukumu la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Serikali ya Mkoa wa Kagera limekamilishwa la kufikisha miundombinu ya Barabara, Maji na Umeme katika eneo hilo ili Serikali ya Watu wa China iweze kuanza ujenzi mara moja.
Mara baada ya kufika katika eneo la Burugo akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera alikagua miundombinu ya Barabara, Maji na Umeme iliyofikishwa katika eneo hilo na Serikali na kusema kuwa sasa jukumu la Serikali limekamilika kwa asilimia 100% na kilichobaki ni Serikali ya Watu wa China kuanza ujenzi mara moja.
“Sisi Serikali ya Tanzania tumekamilisha kila kitu kilichotakiwa kwa upande wetu kilichobaki sasa ni Serikali ya Watu wa China kuanza ujenzi mara moja katika eneo hili ambapo ujenzi huo utagharimu jumla ya Shilingi bilioni 22.4 na chuo hiki kikamilika kitakuwa kinapokea jumla ya wanafunzi 800 wa fani mbalimbali za ufundi stadi kwa wakati mmoja.” Alifafanua Profesa Ndalichako.
Ikumbukwe kuwa Serikali ya Watu wa China mwaka 2015 ilihaidi kutoa shilingi bilioni 22.4 kwa ajili ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Rais Jakaya Kikwete akaagizachuo hicho kijengwe Mkoani Kagera. Ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Kagera unatarajia kuanza mwezi Mei 2019 mara baada ya taratibu za kusaini mikataba na manunuzi kukamilika.
Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako alitembelea ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ufundi Stadi Wilayani Karagwe (Karagwe Development Vocational Training Center KDVTC) ambapo Serikali ilitoa Shilingi bilioni 4.6 ili Chuo hicho kiboreshwe miundombinu yake ya majengo na kujenga majengo mapya ili kiweze kukidhi viwango vya kupokea wanafunzi wengi zaidi.
Ujenzi wa Chuo cha KDVTC unaosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na ngazi ya ujenzi ipo katika hatua ya msingi jambao ambalo lilimfanya Profesa Ndalichako kumwagiza Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Kagera Mhandisi Salum Chanzi anayesimamia ujenzi huo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa muda uliopangwa wa mwaka mmoja ifikapo Julai 2019.
Aidha, katika hatua nyingine Profesa Ndalichako alitembelea Shule ya Sekondari Bukoba na kukagua majengo yaliyoezuliwa na upepo na upepo mkali usiku wa kuamkia tarehe 17.10.2018 pia majengo hayo yakiwa yameathiriwa na Tetemeko la Ardhi la Septemba 10, 2016 na kuhaidi kuendelea na ufuatiliajia wa upatikaji wa fedha ili shule hiyo iweze kukarabatiwa na wananafunzi waliohamishiwa Shule za Sekondari Omumwani na Ihungo waweze kurejea na kuendelea na masomo katika Shule hiyo.
Kwa upande wa maendeleo ya Elimu katika Mkoa wa Kagera Profesa Ndalichako mara baada kupokea taarifa ya mkoa ya maendeleo ya elimu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliupongeza uongozi na wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa kuendelea kufanya vizuri na kuwa katika nafasi kumi bora za mwanzo katika mitihani mbalimbali.
Pia Profesa Ndalichako alisema kuwa mkoa unatakiwa kuzifanyia kazi haraka changamoto za miundombinu katika shule mfano uhaba wa matundu ya vyoo na mlundikano wa wanafunzi katika madarasa. “Chanagamoto ya vyoo inatakiwa kufanyiwa kazi haraka ukizingatiwa kuwa mkoa huu una mvua nyingi jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya watoto wawapo shuleni.” Alisisitiza Profesa Ndalichako.
Mkoa wa Kagera umeendelea kufanya vizuri katika matokeo mbalimbali na kuwa miongoni mwa mikoa kumi bora inayoshika nafasi za juu ambapo kwa miaka mitatu mfurulizo 2016, 2017, na 2018 Mkoa wa Kagera uliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza Kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara katika Mtihani wa Upimaji wa Darasa la Nne.
Matokeo ya Darasa la Saba Kitaifa mwaka 2016 Kagera ilishika nafasi ya 5, Mwaka 2017 nafasi ya 3 na mwaka 2018 nafasi ya 5 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Katika Mtihani wa Upimaji wa Kidato cha Pili Kitaifa kwa mwaka 2016 Kagera ilishika nafasi ya 4, Mwaka 2017 nafasi ya 6 na mwaka 2018 nafasi ya 7 kati ya mikoa 31 ya Tanzania Bara na Visiwani.
Aidha, Katika Matokeo ya Mtihni wa Taifa wa Kidato cha nne Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2016 ilishika nafasi ya 3, Mwaka 2017 nafasi ya 9 na mwaka 2018 nafasi ya 8 Kitaifa kati ya mikoa 31 ya Tanzania Bara na Visiwani. Shule ya Kemebos iliyopo Manispaa ya Bukoba ilishika nafasi ya 2 Kitaifa mwaka 2018.
Pamoja na Mkoa wa Kagera kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2018 lakini Shule ya Sekondari Rwemondo iliyopo Wilayani Missenyi ilishika nafasi ya 4 kwa shule kumi za mwisho jambo ambalo linapelekea kengere kulia kwa uongozi wa Wilaya pia na Mkoa kuiangalia shule hiyo kwa jicho la tatu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
Anwani: S.L.P 299 BUKOBA
Simu ya Mezani: 255 28 2220215/17
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras.kagera@tamisemi.go.tz
Haki zote zimehifadhiwa